Malori yakwama mpakani Kenya-Tanzania siku 30

13Oct 2021
Hamida Kamchalla
Dar es Salaam
Nipashe
Malori yakwama mpakani Kenya-Tanzania siku 30

MADEREVA wa malori ya mizigo yanayosafirisha mazao kama mahindi na mbao kutoka nchini kwenda nchi jirani ya Kenya, wamelalamika kusota mpakani kwa takribani mwezi mmoja, wakidai kusubiri kufanyiwa ukaguzi.

Kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya madereva waliozungumza na Nipashe, walisema tangu walipofika mpaka wa Lungalunga nchini Kenya ni muda mrefu umepita wakisubiri ukaguzi huo, lakini hawajafanikiwa kuruhusiwa kuondoka.

Mwakilishi wa madereva hao, Nassoro Ally kutoka Mkoa wa Iringa, alisema usumbufu huo umesababisha waishiwe fedha za matumizi, jambo ambalo limewaathiri kiuchumi.

“Mpaka sasa hatujapatiwa taarifa yoyote kuhusiana na mkwamo huu, ingawa tukiri kwamba kuna ukaguzi unafanyika kwa malori machache kwa siku tofauti na awali. Kwa siku wanakagua malori zaidi ya 30.

“Sisi wengine, tuna zaidi ya mwezi tupo tu, pesa za kutumia zinatuishia na hatujui hatma yetu mpaka muda huu.
Hatujakaguliwa na ukiingia humo ndani hakuna majibu ya kueleweka, yaani hata ukaguzi wenyewe unafanywa kwa kusuasua. Kwa siku wanaweza kukagua malori manne yanavuka kuingia Lungalunga, wengine tunaendea kusota hapa na hatujui hatma yetu.”

Nipashe ilifanikiwa kuzungumza na Ofisa Mfawidhi wa Forodha wa Kituo cha Pamoja cha Horohoro, Mohamed Shamte, alisema malori yaliyoko nje ya lango yakisubiri kuvuka kwenda nchini Kenya, yanasubiri kufanyiwa ukaguzi kutoka upande wa Lungalunga, ambako wamedai wanamabadiliko katika mfumo wa afya.

Kwa mujibu wa Shamte, wao katika Kituo cha Horohoro, hawana tatizo na kwamba kwa sasa hakuna mizigo ya kukagua, pia katika sehemu yao ya kuegeshea magari na wala hakuna malori ya mizigo, ambayo yanasubiria huduma zao.

“Tunafanya ukaguzi si chini ya lori 30 kwa siku, kwa mizigo mbalimbali, ukikuta lori limesimama hapa (Horohoro), ujue lina shida nyingine tu. Tunafanya ukaguzi kwa kila gari linaloingia ndani ya siku moja na ndio maana sina gari hapo.

Utaona hayo yaliyopo hapo yanaenda mataifa mengine, hayo magari yaliyosimama hapo nje yanakwenda Kenya na hizo bidhaa tayari ni za Wakenya. Sasa utashangaa kwa nini wanachelewesha mali ya kwao wenyewe.

Zaidi alifafanua: “Sisi kama Watanzania tumeshawauzia Wakenya bidhaa na wao wana wajibu kwa taifa lao na huo wajibu upo kisheria na kuna hatua, ambazo zinatakiwa zifuatwe, ili ziweze kukamilika, sasa wakifuata zile hatua katika utaratibu ambao umekamilika mzigo unatoka, sasa ukiona mzigo hauendi ujue kuna shida.”

Hata hivyo, Shamte alisisitiza kuwa kituo hicho kimepiga hatua kubwa hasa kwa upande wa ukusanyaji wa tozo za mizigo, baada ya kujiwekea lengo la kukusanya Sh. bilioni 9, lakini wamevuka lengo hilo kwa kukusanya Sh.bilioni 11, ambayo ni sawa na asilimia 120.

Vilevile, Nipashe ilifanikiwa kuzungumza na Ofisa Mfawidhi wa Forodha wa Kituo cha Lungalunga, aliyejitambulisha kwa jina moja la Musiri, ambaye alikiri kuwapo kwa mabadiliko hayo, lakini hakuthibitisha kama ndiyo chanzo cha malori kusota katika kituo chao.

Habari Kubwa