Manispaa yapata vifaa kumaliza tatizo la taka

27Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Tabora
Nipashe Jumapili
Manispaa yapata vifaa kumaliza tatizo la taka

JUMLA ya shilingi milioni 334 zimetumiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kununua gari la kubeba taka na makontena 20 ya kuweka takataka hizo.

Taarifa hiyo ilitolewa jana na Fundi Mkuu wa Manispaa ya Tabora Gaitan Mkweng’e wakati wa mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani wa kuzungumzia bajeti.

 

Alisema kuwa gari ni jipya ambalo limenunuliwa kutoka China na kwamba litasaidia kukusanya na kuondoa taka katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Tabora.

 

 Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Tabora Bosco Nduguru, alisema uzalishaji wa taka kwa siku katika manispaa hiyo ni tani 120 lakini kabla ya ununuzi wa gari hilo walikuwa na uwezo wa kukusanya tani 70 pekee.

 

Alisema ununuzi wa gari hilo utawezesha manispaa hiyo kuwa na uwezo kumalizia sehemu ya taka ambayo ilikuwa inabaki kwa siku.

 

Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira wa Manispaa  William Mpangala alisema ununuzi wa gari utasaidia sana kwani kila tarafa itakuwa na gari lake na ukusanyaji wa taka utaimarika.

 

Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Cheyo, Hamisi Kitumbo alisema ununuzi wa gari jingine utawezesha wakazi wa halmashauri hiyo kuishi katika mazingira safi na salama.

 

Alisema hatua hiyo itapunguza kuwepo na uwezekano kwa magonjwa ya mlipuko yanayotokana na mrundikano wa uchafu katika maeneo yasiyo rasmi kwa ajili ya kutupa taka.

 

 

Habari Kubwa