Manyara yatangaza bei kikomo ya mbaazi

23Sep 2016
John Ngunge
Nipashe
Manyara yatangaza bei kikomo ya mbaazi

BAADA ya wakulima kukosa soko la uhakika la mbaazi, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk. Joel Bendera, ameingilia kati na kuweka bei elekezi ya zao hilo.

Bei iliyotangazwa ni Sh. 1,200 kwa kilo badala ya Sh. 800 ya awali. Kutokana na kukosa soko la zao hilo, baadhi ya wakulima walisusa kuvuna mbaazi na kuziacha mashambani zikiharibika.

Akizungumza mjini hapa jana, Dk. Bendera alisema bei elekezi inapaswa kufuatwa na wanunuzi na wakulima wote wa zao la mbaazi ambalo kwa namna moja au nyingine limewanufaisha wakulima wa mkoa huo kwa msimu uliopita.

Aliwataka wanunuzi wote kufuata bei hiyo elekezi kwa kuwa kikao cha maridhiano kilikubaliana na kuipanga kwa ajili ya kuwasaidia wakulima ambao wengi wao walikuwa wanazitelekeza mbaazi mashambani.

Hata hivyo, alisema mnunuzi atakayekuja na bei nzuri zaidi, serikali itampunguzia gharama zingine zitakazoongezeka wakati wa kukusanya zao hilo.

Alisema kwa wale waliopanga bei zao chini ya bei elekezi watachukuliwa hatua. Aliziagiza mamlaka husika kushirikiana na viongozi wa halmashauri za wilaya, tarafa, kata na vijiji, kuhakikisha zinawadhibiti wanunuzi wote watakaokiuka utaratibu uliowekwa hasa bei hiyo elekezi kwa wakulima wa mbaazi.

Alisema wanapofikiria kumwezesha mkulima, wasijifikirie peke yako bali wanapaswa kumwangalia mkulima huyo ambaye hana shughuli nyingine za kujiingizia kipato na kuendesha maisha yake zaidi ya kulima mazao na kisha kuyauza apate riziki.

Kwa upande wake, mnunuzi wa zao hilo, Januari Mohamed, alisema bei ya mbaazi itazidi kupanda kadri watakavyokuwa wanainunua kwa wakulima kwa kuwa msimu huu inaonyesha mavuno yamekuwa mengi.

Habari Kubwa