Maofisa kilimo, ugani wafundwa

25Feb 2021
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Maofisa kilimo, ugani wafundwa

MAOFISA kilimo na mabwana shamba wametakiwa kuwasimamia wakulima katika maeneo yao, ili kulima kitaalamu na kufikia malengo ya kujitosheleza kiuzalishaji.

Hayo yalisemwa jana mjini Zanzibar na mshauri wa utaalamu wa mipango wa kilimo hai kutoka Wizara ya Kilimo, Omar Abubakar, wakati akifunga mafunzo ya siku tano ya kilimo cha viungo kwa maofisa wa kilimo.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeweka kipaumbele katika sekta ya kilimo ili kuwainua wakulima na kuongeza uzalishaji.

Alisema ni wajibu wa wataalamu hao kuhakikisha wanatoa mafunzo bora kwa wakulima ili kuwaingiza katika kilimo cha kisasa na chenye tija kitakachotoa mazao mengi na yenye ubora. 

Mazao ya viungo, alisema yana soko kubwa kitaifa na kimataifa, hivyo ni vyema wakulima kuzidisha bidii katika kilimo hicho ili kuwapatia tija.

“Kilimo kizuri cha viungo na chenye soko ni kile kilimo hai ambapo mazao yake huwa ni mazuri zaidi kiafya,” alisema.

Alisema Wizara ya Kilimo kupitia mradi wa kilimo cha viungo, imekusudia kuwaorodhesha wakulima hao ili kuhakikisha wananufaika na mipango wa kuwaendeleza kiuchumi. 

Kwa upande wao maofisa hao wa kilimo waliiomba Wizara ya Kilimo kufuatilia changamoto zinazowakumba wakulima katika miradi mbalimbali inayoanzishwa ili iwe fursa ya kuzitafutia ufumbuzi na kuanzishwa miradi mipya.

Mafunzo hayo yaliiyotayarishwa kwa pamoja kati ya Wizara ya Kilimo, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Ofisi ya Zanzibar na People’s Development Forum (PDF) yanalenga kuwawapatia  wakulima wa viungo  mbinu za kisasa za kilimo hicho zitakazowaongezea uzalishaji na kupata masoko ya uhakika.
 

 

Habari Kubwa