Maofisa ugani washauri wakulima kufunzwa mbinu

22Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Njombe
Nipashe
Maofisa ugani washauri wakulima kufunzwa mbinu

MAOFISA ugani wastaafu wamehimiza wakulima wafunzwe kulinda afya ya udongo, juhudi ambayo inafanywa hivi sasa kukuza matumizi ya mbolea asilia ili kuinua tija katika sekta ya kilimo.

Baadhi ya maofisa ugani wastaafu wameeleza kufurahishwa na jitihada inayoofanywa wakati huu kupambana na tindikali ardhini ambayo inachakaza ardhi na kupunguza sana mavuno.

Wakuzungumzia mbolea ya kukuza kilimohai iliyozinduliwa mjini hapa, wamesifu utengenezaji wa mbolea hiyo, lakini wamehimiza pia matumizi ya mbolea zinazotokana na wanyama na mimea. 

Ofisa ugani mstaafu, Florence Mapunda, alisema kuna haja ya kuwaelimisha wakulimu juu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa sababu watu wengi wana elimu.

Ofisa Mstaafu, Gerald Mhagama, alipendekeza vyuo vikuu, vyuo vya mafunzo ya kilimo na taasisi za utafiti na maofisa ugani wafanye juhudi ya pamoja kuwafundisha wakulima juu ya matumizi ya mbolea. 

Erasto Ngole, mkulima wa parachichi mkoani Njombe, alisema kuwa alianza kutumia mbolea ya hakika toka ikiwa katika hatua ya majaribio, na kueleza kwamba kwa kutumia mbolea hiyo anavuna kutoka kwenye mti mmoja wenye afya matunda makubwa na kupata Sh. milioni 1.2. 

Esther Msigwa, mkulima wa Wilaya ya Wangingombe, alisema anafarijika kuona anapata mazao mengi kwa sababu ya kutumia mbolea ya kisasa. Nina shamba ekari moja na wamenifundisha namna nzuri ya kutumia mbolea hii. Matokeo ni mazuri,” alisema. 

Wakala wa pembejeo za kilimo wa Rungwe, mkoani Mbeya, Daniel Mwakipesile, alisema wakulima wanaelekea kuipenda mbolea ya hakika na kwamba ataendelea kuwa msambazaji wa mbolea hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mbolea hiyo hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Guavay ambao ndio wazalishaji wa mbolea hiyo, Mhandisi Ahad Katera, alisema wamejipanga kuongeza uzalishaji kutoka tani 3,500  mpaka kufikia tani 20,000 kwa mwaka ili kukidhi mahitaji kwa wakulima.

Utafiti wa mbolea hiyo ulianza mwaka 2014 na kukamilika mwaka 2017 na ulishirikisha Chuo Kikuu Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Chuo Kikuu cha Makerere, Tume ya Sayansi na Teknolojia na wadau wengine kupitia ufadhili wa Shirika la Bolnnnovate Afrika lenye makao makuu yake Nairobi, Kenya.

Habari Kubwa