Maonyesho ya madini yatajwa kuwa na tija

28Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Maonyesho ya madini yatajwa kuwa na tija

MAONYESHO ya madini na teknolojia yaliyomalizika jana mkoani Geita, yametajwa kuwa na tija kubwa kwa wadau wa sekta ya madini na serikali.

Hayo yameelezwa na Benki ya NBC ambayo ilikuwa miongoni mwa taasisi zilizoratibu maonyesho hayo, na kueleza mkakati wake wa kutekeleza kwa vitendo masuala muhimu iliyoahidi kuyafanya kwa kushirikiana na wadau hao ili kuboresha zaidi sekta hiyo.

Akitoa tathmini ya ushiriki wake katika maonyesho hayo yaliyofungwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki, aliyemwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Mkurugenzi wa Idara ya wateja binafsi wa benki hiyo,  Makao Makuu, Elibariki Masuke, alisema katika kipindi chote cha maonyesho hayo, benki hiyo ilifanikiwa kuendesha programu mbalimbali ikiwamo mafunzo kwa wadau takribani 600 wa sekta ya madini wakiwamo wachimbaji wadogo na wajasiriamali.

“Pia mbali na huduma za kibenki ikiwamo kufungua akaunti mpya kwa wateja, tumefanikiwa kuendesha kliniki za biashara ambapo tuliweza kuwakutanisha wafanyabiashara na taasisi au mamlaka mbalimbali zinazogusa biashara zao. Zaidi, kupitia makongamano mbalimbali tumewawezesha wadau wa sekta ya madini kubadilishana mawazo baina yao wenyewe, lakini baina yao na mamlaka mbalimbali za serikali ikiwamo Wizara ya Madini, TRA, NEMC, SIDO na TANTRADE, TABWA, OSHA, GST na NSSF,’’ alisema.

Aliongeza kuwa ili kuhakikisha mafunzo yaliyotolewa na taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine yanaleta tija iliyokusudiwa kwa wadau wa sekta ya madini, benki hiyo inaandaa mkakati wa utekelezaji wa masuala muhimu yaliyoafikiwa ikiwamo kuja na huduma maalum ya kibenki mahususi kwa ajili ya wadau wa sekta ya madini.

Kwa upande wake Meneja Uhusiano na Serikali wa Benki hiyo, William Kallaghe, alisema kupitia maonyesho haya benki hiyo imeweza kujadiliana na serikali pamoja na kampuni kubwa ikiwamo migodi mikubwa ambapo kwa pamoja wameona umuhimu wa kampuni hizo kutoa mikataba ya kisheria kwa wazabuni wao, ili kupitia huduma ya mikopo isiyo na dhamana inayotolewa na benki hiyo iweze kuitumia mikataba hiyo kuwakopesha zaidi wazabuni hao.

Kufuatia maelezo hayo Waziri Kairuki aliiagiza benki hiyo kuhakikisha inawasilisha maoni yote ya wadau wa sekta ya sekta madini yaliyokusanywa kupitia Kliniki ya Biashara ya benki hiyo na iyawasilishe kwenye ofisi yake kwa kushirikiana na Wizara ya Madini ili yaweze kufanyika kazi.

Habari Kubwa