Marekani yajitosa kusaidia wakulima kahawa

20Mar 2019
Godfrey Mushi
Moshi
Nipashe
Marekani yajitosa kusaidia wakulima kahawa

MFUKO wa Maendeleo wa Marekani unaohudumia nchi za Afrika (USDF), umejitosa kuwatoa kimasomaso wakulima zaidi ya 800 wa kahawa katika eneo la Kinyamvuo, Wilaya ya Moshi, baada ya kukubali kugharamia pembejeo za kilimo na miche bora.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Kinyamvuo, Felix Mlay, zimeeleza kuwa pembejeo hizo zitatolewa kwa bei nafuu zaidi ili kukabiliana na walanguzi wa pembejeo.

Mlay alisema miche hiyo na pembejeo zimetolewa na Shirika la USDF ambalo lina lengo la kuboresha kilimo cha zao hilo na kufanikisha malengo ya serikali ya kuongeza uzalishaji.

Mlay alisema tayari wamepewa zaidi ya Sh. milioni 200 na shirika hilo kwa ajili ya kununua miche, kukarabati ofisi na ghala la kuhifadhia kahawa.

Fedha hizo pamoja na mambo mengine zitatumika kununua pembejeo ambazo wataziuza kwa bei nafuu kwa wakulima na kuwawezesha kulima kilimo bora cha kahawa na kuondokana na kilimo cha mazoea.

"Wakulima watapata pembejeo na zinaweza kutolewa kwa mkopo na baadaye mkulima akalipa kutokana na kahawa atakayouza, lakini pia miche mingi ya kahawa imezeeka, na tumepewa fedha kwa ajili ya kununua miche bora, hii ni fursa kubwa kwetu katika kuboresha kilimo hiki ambacho wengi walishakikatia tamaa," alisema Mlay.

Daudi Mariki ambaye ni mkulima wa kahawa katika kijiji hicho, aliwataka wakulima wenzake, kutumia fursa hiyo kuboresha kilimo cha kahawa, na kufanikiwa kujikwamua kiuchumia kupitia kilimo cha zao hilo.

"Tunaishukuru serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikiweka mikakati ya kuboresha zao hili na hata kutuletea wafadhili, ni vizuri sasa wakulima tukajituma katika kazi na kutumia wataalamu tulio nao kuboresha zao hili," alisema Mariki.

Ofisa Ugani wa Kijiji cha Mwika Kinyamvuo, Devotha Assenga, alisema wameendelea kutoa elimu kwa wakulima kubadilisha miti ya kahawa ya zamani na kupanda miche mipya inayotoka Taasisi ya Utafiti wa Kahawa nchini TaCRI, ambayo haishambuliwi na magonjwa.

"Tumeshaandika barua TaCRI (Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania), kuomba miche ambayo haishambuliwi na magonjwa ya chulebuni na kutu ya majani.

"Na mpaka sasa wana mpango wa kutuletea miche 1,500, na tunaendelea kuelimisha wakulima kubadilisha kahawa ya zamani ili kufanikiwa kulima kahawa bora na yenye tija."