Marekani yasaidia kutungwa kanuni sheria wanyamapori

25Jun 2019
Salome Kitomari
Nipashe
Marekani yasaidia kutungwa kanuni sheria wanyamapori

SHIRIKA la Misaada la Marekani (Usaid), limeisaidia serikali kukamilisha kanuni za sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009 ambayo pamoja na mambo mengine, inalinda mapito ya wanyamapori maarufu kama shoroba.

Aidha, Usaid kupitia ‘Usaid Project’ iko kwenye mazungumzo na Mamlaka ya Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri), ili kufanya utafiti mwingine wa hali ya  shoroba baada ya utafiti wa mwaka 2009 ambao uliainisha uhai wa kila shoroba na kuonyesha ifikapo 2050 zitabaki shoroba mbili.

Shoroba ni mapito ya wanyama kutoka hifadhi moja hadi nyingine kwa ajili ya kutafuta mahitaji yao ikiwamo kwenda maeneo ya mtawanyiko kwa ajili ya kuzaliana na kupata madini muhimu kwa ajili ya miili yao.

Sheria ya Wanyamapori inayosimamia sekta hiyo ni ya mwaka 2009 na toka wakati huo hakukuwa na kanuni ambayo pamoja na mambo mengine inataja ukubwa na namna ya kutunza shoroba ambazo nyingi zimeshavamiwa na shughuli za kibinadamu.

Akizungumza hivi karibuni na Nipashe, Mtaalamu wa Usimamizi wa Maliasili na Sera wa Usaid Protect, Exper Pius, alisema mkutano wa wadau ulifanyika mwaka 2017 na walitoa maoni.

Alisema mchakato ulisimama kwa muda baada ya mabadiliko ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ambaye alitia saini kanuni hizo Machi 16, mwaka jana, ambazo zitasimamia uanzishwaji wa shoroba.

"Kanuni inatambua kuwa maeneo hayo ni ya wananchi, inabidi serikali izungumze na wananchi ili ziwapo na maeneo husika yasibadilishwe hadhi ya umiliki isipokuwa matumizi," alisema.

Alisema kwenye kanuni wananchi watatakiwa kutumia maeneo yao ambayo yanakutwa na shoroba kwa muundo wa uhifadhi endelevu kwa maana ya kuruhusu wanyama kupita wakati wakiendelea na shughuli zao.

"Kazi wanazoweza kufanya ni kama kuchunga mifugo yao na nyingine ambazo haziwezi kuleta mgongano na wanyamapori, mfano wakilima mazao ambayo wanyama watayala moja kwa moja wataingia kwenye mgogoro na wanyama," alisema.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, baada ya kanuni kuwepo kuna mambo ya msingi yanatakiwa kufanyika kutokana na maoni ya wadau kuwa kuna mambo ya msingi hayakufanyika.

"Tumeamua kuisaidia serikali kuanzisha mchakato wa kuzitambua shoroba hizo kwa kutumia taratibu zilizopo kwenye kanuni ili kuona mabadiliko kabla ya kutumika rasmi maeneo yote nchini," alisema.

Pius alisema majaribio ya kanuni hizo yanafanyika kwenye shoroba ya Magombera Mwenehana inayounganisha Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa na eneo la asili la Hifadhi ya Magombera hadi Pori la Akiba la Selous, ambayo inapita kwenye eneo lililohifadhiwa la Kwakuchinja.

Alisema uwepo wa maeneo ya hifadhi ya jamii yaani Wildlife Management Area (WMA), kunasaidia kuendelea kuwepo kwa shoroba na kutunza hifadhi dhidi ya uvamizi.

"Lazima tuzitambue shoroba husika kwa kuwa kuna ambazo zimeshakufa kutokana na shughuli za binadamu kwa maana ya mashamba, nyumba na kwa sasa wanyama hawawezi kupita kutoka eneo moja kwenda jingine," alisema.

Mwaka 2017, Nipashe ilifanya habari ya uchunguzi juu ya hali ya shoroba na kubaini kuwa baadhi ya hifadhi kama Hifadhi ya Taifa ya Arusha (Anapa), imebaki kisiwa kutokana na shoroba kuvamiwa na shughuli za kibinadamu na sababu kubwa ni kukosekana kwa kanuni ya sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009.

Utafiti uliofanywa na Tawiri mwaka 2009, unaonyesha kuwa uvamizi wa shoroba umesababisha wanyama kuuawa, uwindaji haramu na kusambaa kwa magonjwa ya wanyamapori kwenda kwa wanyama wa kufugwa na kinyume chake pamoja na baadhi ya maeneo yaliyohifadhiwa kuwa kisiwa na wanyama kuzaliana aina hiyo hiyo ambayo ni rahisi kufa kwa ugonjwa au kuwa dhaifu.

Habari Kubwa