Marekebisho Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa yaja

21Jan 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Marekebisho Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa yaja

OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), imesema ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290, ili kuongeza usimamizi na ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Waziri wa Nchi wa Ofisi hiyo, Selemani Jafo.

Sheria hiyo inaainisha mamlaka na taratibu mbalimbali zinazohusu usimamizi wa fedha kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na pia vyanzo mbalimbali vya mapato.

Hayo yalibainishwa juzi na Waziri wa Nchi wa Ofisi hiyo, Selemani Jafo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini hapo kuhusu taarifa ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa kipindi cha nusu ya mwaka (Julai-Desemba) 2018/19.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuondokana na changamoto za ukusanyaji mapato ya ndani kwa mamlaka hizo.

"Sheria hiyo imetumika kwa muda mrefu tangu 1982 hivyo, marekebisho hayo yanalenga kuweka uhalisia wa utendaji wa sasa katika namna bora zaidi ya usimamizi na ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa," alisema.

Aidha, Waziri Jafo alisema katika kipindi cha nusu mwaka, halmashauri zimekumbana na changamoto mbalimbali ikiwamo baadhi ya wanunuzi kuchelewa kulipa ushuru kwa halmashauri na kusababisha kuonekana zimekusanya chini ya kiwango.

"Pia baadhi ya halmashauri kutegemea zaidi chanzo kimoja na kushindwa kukusanya kutoka kwenye chanzo hicho kunaweza kusababisha halmashauri hizo kushindwa kujiendesha," alisema.

Kadhalika, alisema kuna matumizi mabovu ya mifumo ya kukusanyia mapato kwa njia za kielektroniki kwa baadhi ya halmashauri, kutumia takwimu za makisio zisizo uhalisia na kushindwa kuweka mikakati madhubuti ya kukusanya mapato kutoka kwenye vyanzo vipya vinavyobuniwa na halmashauri.

Aidha, Waziri Jafo alisema wameweka mikakati mbalimbali ya kutatua changamoto hizo na kusisitiza ofisi yake itaendelea kuzisimamia kwa karibu halmashauri zote zinazoonyesha kusuasua katika suala la ukusanyaji wa mapato.

Aliitaka mikoa na halmashauri kusimamia utoaji wa taarifa kupitia mifumo ya kielektroniki ikiwamo kazi za usuluhishi na kusafisha takwimu chafu kwenye mfumo wa Epicor 10.2, ili kuwezesha kuwa na takwimu sahihi kwenye ‘Dashboard’ ya mapato ya ndani na kwa wakati.

Pia alisema ofisi yake imeandaa mwongozo wa ukusanyaji mapato ya ndani ili kuzisaidia halmashauri kuwa na uelewa wa pamoja kwa watu wote ya masuala ya ukusanyaji wa mapato kuanzia suala la kupanga, kukadiria, kukusanya, kutumia, ukaguzi wa nje na ndani na kutoa taarifa.