Marufuku kuchanganya korosho, mchanga, kokoto

22Oct 2018
Hamisi Nasiri
Masasi
Nipashe
Marufuku kuchanganya korosho, mchanga, kokoto

MKUU wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Selemani Mzee, amewapiga marufuku wakulima wa zao la korosho kuacha kuchanganya korosho, mchanga na kokoto kwenye magunia kwa lengo la kuongeza uzito wa kilo za zao hilo kisha kwenda kuzipima ghalani.

MKUU wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Selemani Mzee picha na mtandao

Aidha, amepiga marufuku malori yanayosafirisha magunia ya korosho kutosafirisha mizigo hiyo usiku, ili kupunguza wizi wa magunia ya korosho unaofanywa na baadhi ya madereva wa malori hayo.

Alisema katika msimu huu wa korosho serikali yapo mambo ambayo yamepewa kipaumbele katika kuyasimamia hadi pale msimu utakapokuwa umemalizika.

Aliyataja baadhi ya mambo hayo ni wakulima kuchanganya korosho, mchanga na kokoto kwenye magunia ya korosho kwa lengo la kuongeza uzito kabla ya kwenda kupima kwenye maghala.

Mzee alieleza kuwa mkulima ambaye magunia yake ya korosho yatakutwa yakiwa yamechanganywa na korosho, mchanga na kokoto, mzigo wake wa korosho utataifishwa na mhusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha korosho zote zinazouzwa na wakulima kwenye minada na kupelekwa kwenye maghala zikiwa safi, hivyo kila mkulima lazima awe makini.

Alisema katika msimu serikali imeamua kuweka utaratibu wa muda wa kusafirisha korosho ambao ni saa 12:00 jioni na atakayekutwa akisafirisha korosho zaidi ya muda huo, atakamatwa na korosho zote kutaifishwa na kwamba lengo la utaratibu huo kwa mwaka huu ni kupunguza wizi wa korosho za wakulima.

“Masasi hatuna sifa ya kuwa na korosho chafu ambazo zinakuwa zimechanganywa na michanga na kokoto. Nisingependa kuona mkulima yeyote anajaribu kuweka mchanga au kokoto kwenye magunia yake ya korosho kwa lengo la kuongeza uzito wa korosho, tutamchukulia hatua kali za kisheria,” alisema Mzee.

Aidha, Mzee alisema serikali inasisitiza makarani wote wanaohusika kulipa fedha za wakulima kuwa makini katika kuwalipa, ili makosa ambayo katika msimu uliopita yalikuwapo yasijitokeza tena na kwamba hata taasisi za kifedha zimeshapewa angalizo la kuwa makini na fedha za wakulima.

Alisema zimebaki siku chache kabla ya minada kuanza, hivyo wakulima wapeleke korosho kwa wingi maghalani kuziuza na kwamba hakuna sababu kwa mkulima kuuza korosho zake kwa njia ‘chomachoma’ kwa sababu hupata fedha kiduchu ukilinganisha na kuuza kwa njia rasmi ya mfumo ya stakabadhi mazao ghalani.

Mbunge wa Masasi, Rashidi Chuachua, alisema vyama vya msingi vikumbuke madeni ya wakulima ya msimu uliopita, hivyo watakapopata fedha za malipo ya msimu huu, ni lazima wawalipe wakulima wote ambao wanadai fedha kwa kuwa msimu uliopita baadhi ya vyama havikuwalipa wakulima wake.

Alisema katika msimu wa mwaka jana wakulima katika vyama vya msingi vilivyopo Halmashauri ya Mji wa Masasi walikuwa hawajalipwa hadi sasa kufikia msimu huu wa 2018/19
wanadai zaidi ya Sh. milioni 197.

Habari Kubwa