Marufuku kufunga nyama kwa magazeti

30May 2019
Mary Mosha
MOSHI
Nipashe
Marufuku kufunga nyama kwa magazeti


MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Anna Mghwira, amepiga marufuku wauza nyama mkoani humo kufunga kitoweo hicho kwenye magazeti.

Aidha, amewaonya kuwa magazeti yana athari kwa afya za walaji.

Agizo hilo ni kufuatia maelekezo ya Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa, alilolitoa Aprili 29, mwaka huu,

 kukataza mifuko ya plastiki kutumiwa nchini kutokana na madhara kwa binadamu na mazingira.

Alisema kuwa amepokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa wauza nyama wanatumia magazeti kufungia nyama hali ambayo inaharatisha afya zao.

“Wananchi wamekuwa wakilalamika kuwa wanafungiwa nyama kwenye magazeti ambayo yana sumu, kwani wino unaotumiwa kuchapisha taarifa hizo haufai kuliwa.”

Aliongeza kuwa kama mkoa wameagiza wauza nyama waache mara moja na  watumie mifuko au vifungashio rafiki wa mazingira.

Mkuu wa Mkoa, Dk. Mghwira, alisema watu wenye mzigo au bidhaa nyingi za mifuko yote ya plastiki iwasilishwe kwenye halmashauri na kuwekewa kumbukumbu ili  kusubiri maelekezo ya wataalamu hasa kuitumia kwa matumizi mengine.

“Wale wote wenye mifuko ya plastiki kwa kiwango kikubwa waiwasilishe kwenye halmashauri ili iweze kutumika kwa matumizi mengine kuepuka uchafuzi wa mazingira tutafuata maelekezo na ushauri wa wataalamu wetu.”

Mbali na hilo alisema kuwa mifuko ya plastiki iliyotupwa katika majalala iwe imeokotwa yote na kuhifadhiwa sehemu maalumu na hairuhusiwi mwananchi kuendelea kuitupa mifuko hiyo na atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Aliwataka Shirika la Viwango nchini (TBS) kutoa ufafanuzi sahihi kwa wananchi juu ya mifuko mbadala ambayo inakidhi vigezo na isiyo na madhara kwa wananchi na rafiki wa mazingira.

Alisema: “Kuna aina nyingi za mifuko mbadala ambayo imeleta mkanganyiko kwa wananchi. Alitaka ufafanuzi sahihi utolewe kwani mingine inaonekana kuwa ni mizuri lakini si rafiki wa mazingira,” alisema.

Samwel Gideon, akitoa maoni yake aliiambia Nipashe kuwa, kufuatia agizo la Waziri Mkuu ni wakati wa watendaji hasa Idara ya Mazingira kuendelea kutoa elimu ya kina juu ya matumizi sahihi ya mifuko mbadala.

Aisha Mohamed mfanyabiashara wa soko la Mbuyuni, katika Manispaa ya Moshi alisema, ipo haja ya watendaji kufanya kazi kwa bidii kwani wapo wafanyabiashara ambao si waaminifu.

Alisema kuna uwezekano wa baadhi yao kuleta mifuko isiyo rafiki wa mazingira kutoka nchi jirani ili kudai fidia.

Akiwa katika Mkoa wa Kilimanjaro Waziri wa Biashara na Viwanda, Joseph Kakunda, alivitaka viwanda vikubwa na vidogo kuhakikisha vinaongeza uzalishaji wa mifuko mbadala kwani upo uhitaji mkubwa kwa sasa.

“Zipo tetesi kuwa baadhi ya wafanyabiashara ambao sio waaminifu wanatumia fursa hii kuingiza mifuko inayofanana na hii, lakini ndani yake kunachembechembe za plastiki hatutawavumilia na hatua kali za kisheria zitachukulia,” alisema Waziri Kakunda.

Habari Kubwa