Marufuku mgodi North Mara kutumia bwawa la tope sumu

23Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
TARIME
Nipashe
Marufuku mgodi North Mara kutumia bwawa la tope sumu

BARAZA la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC), limesitisha matumizi ya bwawa la kuhifadhia tope sumu katika Mgodi wa Acacia North Mara baada ya sampuli mbalimbali za vipimo kuonyesha kuwa bado kuna utiririshaji wa maji yenye kemikali sumu.

bwawa la tope sumu.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea bwawa hilo lililopo eneo la Nyamongo mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa  NEMC, Mhandisi Dk. Samuel Gwamaka, amesema kampuni imeshindwa kudhibiti utiririshaji wa maji hayo yenye kemikali za sumu zinazototililika kuelekea katika makazi ya wananchi na kuathiri mazingira pia.

“Kama NEMC tumesimamisha matumizi ya bwala la tope sumu mpaka pale watakapoweza kudhibiti utiririshaji wa maji yake au kujenga bwawa jingine jipya ambalo litaweza kudhibiti utiririshaji maji ya kemikali za sumu na kuathiri mazingira na afya za wananchi,” alisema Dk. Gwamaka.

Akiwa ameambatana na maofisa waandamizi kutoka Tume ya Madini, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na pia Baraza, Dk. Gwamaka amesema NEMC haitamwonea aibu wala huruma mtu au kampuni yoyote inayofanya shughuli zake bila kufuata kanuni na taratibu za kimazingira.

“Mfano Bwawa la kuhifadhia tope sumu, Septemba 2018, Februari, Machi, Mei na Juni mwaka huu mwaka huu wataalamu walichukua sampuli katika bwawa hilo na zote zilibaini kuwapo na kemikali zenye sumu,” alisisitiza.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serilikali, Boniventure Masambu, alisema sampuli zote zililizochukuliwa kwa nyakati tofauti na kufanyiwa uchunguzi zimeonyesha kuwapo kwa kemili na hivyo kutoa ushauri.

“Tumefurahi kuona ushauri wetu umefanyiwa kazi mara moja na mamlaka uhusika,” Masambu alisema na kuongeza afya za wananchi na utunzaji wa mazingira ni muhimu kwa mustakabali wa taifa.

Naye Kaimu Meneja wa Acacia, Reuben Ngusaro, aliahidi kufanyia kazi maelekezo yaliyotolewa ilikuweza kukabiliana na athari zote za kimazingira zinazotoka na tope sumu.

“Tutayafanyia kazi maagizo yote kwani tunathamini afya ya wananchi na mazingira. Yote tuliyoyakuta tutayarekebisha,” alisema.