Marufuku uchimbaji wa mchanga Bunju

02Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Marufuku uchimbaji wa mchanga Bunju

SERIKALI imepiga marufuku utupaji  wa taka  na uchimbaji mchanga kwenye Mto Nyakasangwa uliopo eneo la  Bunju jijini Dar es Salaam, kwa kuwa hatua hiyo imechangia uharibifu na uchafuzi wa mazingira.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki katika eneo hilo,  Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Joseph Malongo akiwa ameambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifala Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),   Dk. Samuel Gwamaka, alipiga marufuku ya shughuli zote hapo ikiwamo utupaji taka na uchimbaji mchanga.

“Shughuli zilizokuwa zikiendelea eneo hili zimechangia uchafuzi na uharibifu wa  mazingira kwani zinakiuka sheria na kanuni za mazingira, hivyo serikali inapiga marufuku shughuli zote ambazo zilikuwa zikifanywa hapa,” alisema.

Mhandisi Malongo aliziagiza  mamlaka za serikali za mitaa kote nchini kuhakikisha hakuna shughuli zozote za kiuchumi zinazofanywa kwenye vyanzo vya mito ndani ya mita 60 na ambazo hazina kibali kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

“Naagiza Mamlaka za serikali za mitaa kote nchini kusimamia mazingira kwa mujibu wa sheria na kuwachukulia hatua kali wale wote watakaokiuka kanuni na taratibu zinazongoza katika kusimamia mazingira,” alisemaMhandisi Malongo.

Mhandisi Malongo alisema wanazo taarifa za uwapo wa taasisi na watu binafsi ambao wamekuwa wakitupa taka katikaeneo hilo la Mto Nyakasangwa, hivyo wamejipanga kuimarisha ulinzi.

“Tunachukua hatua kuanzia sasa ambapo nimemwagiza Mkurugenzi mkuu wa NEMC kuwachukulia hatua mara moja viongozi wa serikali ya mtaa huu wa Boko kwa kufumbia macho uchafuzi uliokuwa unafanywa na pia Jeshi letula Polisi litaimarisha ulinzi katika eneo hili ili kuzuia uchimbaji wa mchanga na utupaji wa taka eneo hili,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Dk. Gwamaka alisema baraza lake litaendelea kuchukua hatua kali na za kisheria dhidi ya watuwanaoharibu mazingira ikiwamo utupaji taka kwenye kingo za mito yotenchini.

“Tutaendelea kuchukua hatua kwa watu na taasisi ambazo zimekuwa zikifumbia macho utunzaji wa mazingira kwa kutumia kanuni na sheria zilizopo ili kuyalinda mazingira kwa faida vizazi vijavyo,” alisema.

Aidha, Dk. Gwamaka alikemea tabia ya baadhi ya watendaji wa kata, kitongoji na mtaa wasiowaaminifu kushirikiana na watu au taasisi kutupa taka na kuchimba mchanga kwa manufaa yao binafsi.

Habari Kubwa