Marufuku ya mifuko ya plastiki hospitali

27Jun 2017
Jumbe Ismaily
IGUNGA                
Nipashe
Marufuku ya mifuko ya plastiki hospitali

IDARA ya Afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora imepiga marufuku wagonjwa wote wanaokwenda kufuata huduma za matibabu au kusalimia wagonjwa katika hospitali ya wilaya hiyo kuingia na mifuko ya plastiki maarufu kwa jina la rambo.

Ofisa Afya wa Halmashauri ya wilaya hiyo, John Masesa, alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kuona mifuko hiyo imekuwa ikitumiwa na baadhi ya watu wanaojisaidia kwenye vyoo vya hospitali hiyo, hivyo kusababisha vyoo kuziba.

 Kwa mujibu wa Masesa, mtu yeyote atayebainika kuingia na mifuko ya plastiki atatozwa faini ya Sh. 50,000 na kuwataka watu wote kuzingatia marufuku hiyo.

 Kwa upande wake, Ofisa Usafi na Mazingira wa Halmashauri hiyo, Fredrick Mnahela, alifafanua kuwa suala la usafi siyo la serikali pekee yake, bali ni la kila mtu na kuongeza kwamba yeyote atakayebainika akitupa taka ovyo, atatozwa faini hiyo au kufikishwa mahakamani.

Mnahela alibainisha kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 Halmashauri hiyo imejipanga kujenga vizimba 13 vya kutunza taka sambamba na kutafuta mzabuni atakayekusanya uchafu kwa ngazi ya kaya na kuzipeleka katika vizimba hivyo.

Habari Kubwa