Mashahidi 10 kutoa ushahidi uhamishaji umiliki wa magari

23Jan 2023
Kulwa Mzee
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mashahidi 10 kutoa ushahidi uhamishaji umiliki wa magari

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kutoa taarifa za uongo mahakamani kuhamisha umiliki wa magari 14 na kujipatia fedha kwa udanganyifu inayomkabili Shabani Cosla na dalali wa mahakama, unatarajia kuita mashahidi 10 na vielelezo 12 kuthibitisha ulaghai.

Wakili wa Serikali, Magreth Kisoka, alidai hayo mwishoni mwa wiki katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala mbele ya Hakimu Mfawidhi, Suzan Kihawa, baada ya kumaliza kuwasomea washtakiwa hoja za awali.

Alidai washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 31 yakiwamo ya kutoa taarifa za uongo 27, kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu, makosa matatu na moja la kujipatia fedha kwa ulaghai.

Wakili alidai katika jumla ya mashtaka hayo mshtakiwa Cosla anakabiliwa na mashtaka 23 ya kutoa taarifa za uongo. Inadaiwa Machi 23, mwaka 2012 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, alitoa taarifa za uongo katika mahakama hiyo kwa kuwasilisha shauri la madai namba 99 la mwaka 2012 akionyesha Kampuni ya Escon Borewall Limited ilisajiliwa Tanzania wakati sio kweli.

 

Katika mashtaka mengine mshtakiwa wa kwanza anadaiwa kati ya mwaka 2012 na 2020 alitoa taarifa za uongo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa ni mmiliki halali wa gari namba T844 AKV aina ya Fuso Truck wakati si kweli.

Mshtakiwa huyo anadai kutoa taarifa za uongo katika mahakama hiyo akionesha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imehamisha umiliki wa magari 14 kutoka kwa Kampuni ya Escon Borewell kwenda kwa Kampuni ya SBJ Borewells na Target Borewells Limited wakati akijua si kweli.

Katika mashtaka ya kutoa taarifa za uongo yanayomkabili mshtakiwa wa pili ambaye ni dalali wa mahakama, Charles Sengo, inadaiwa alionyesha Mariyam Hamadi kanunua magari manne katika mnada kwa jumla ya Sh. 275,000,000 wakati si kweli.

Wakili alidai katika shtaka la 28 la ulaghai, mshtakiwa wa kwanza alijipatia gari lenye namba za usajili T975 BQM aina ya Ashok Leyland lenye thamani ya Sh. milioni 75.

Inadaiwa katika shtaka la 29 na 30 mshtakiwa huyo alijipatia magari mengine mawili yenye namba za usajili T346 CHC lenye thamani ya Sh. 65,000,000 na T344 CHC lenye thamani ya Sh. 60,000,000, yote aina ya Ashok Leyland akionesha yaliuzwa katika mnada wa hadhara kutokana na amri ya mahakama katika shauri namba 99 la mwaka 2015 wakati si kweli.

Shtaka la mwisho anadaiwa Aprili 11, 2019 akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Fahak kwa ulaghai alijipatia Sh. milioni 185 kutoka katika akaunti ya mahakama iliyoko Benki Kuu namba 99212697226 kwenda kwenye akaunti ya kampuni yake namba 0150515062000 akionyesha fedha hizo zilipatikana katika mnada uliofanyika Septemba 11, 2016 wakati si kweli.

Washtakiwa katika maelezo yote walikubali taarifa zao binafsi na kukana maelezo yote ya makosa yao, kesi imepangwa kuanza kusikilizwa Februari 23, mwaka huu.

 

Habari Kubwa