Mashamba yaliyofutiwa milki yote kupitiwa upya

17May 2019
Na Mwandishi Wetu
KILOSA
Nipashe
Mashamba yaliyofutiwa milki yote kupitiwa upya

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amesema serikali kupitia wizara yake itapitia upya mashamba yote yaliyofutwa na Rais katika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Lukuvi alisema hayo jana katika kata ya Chanzulu, wilayani hapa, alipozungumza na wananchi alipokwenda kutatua mgogoro wa ardhi katika wilaya hiyo ikiwa ni jitihada za wizara kumaliza migogoro ya ardhi nchini.

 

Waziri Lukuvi alisema katika maeneo mbalimbali yako mashamba yaliyofutwa na Rais lakini hayajawekewa utaratibu wa kuyatumia, hivyo kutoa fursa kwa wajanja wachache kujigawia na mengine kuyauza kwa wananchi bila kufuata utaratibu.

Alisema katika kuhakikisha mashamba yote yaliyofutwa na Rais katika wilaya ya Kilosa na kuzua mgogoro baina ya wananchi na wamiliki, wizara yake imeamua kupeleka timu kutoka wizarani kwa ajili ya kuyafanyia uhakiki.

Kwa mujibu wa Lukuvi, timu hiyo inajumuisha Kamishna wa Ardhi, Mary Makondo; Kaimu Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani, Samweli Katambi;, Mthamini Mkuu wa Serikali, Evalyne Mugasha; Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Kati, Ezekiel Kitilya; na wataalamu kutoka idara za Mipango Miji wizarani.

Alisema uamuzi wa kwenda na timu kutoka wizarani unalenga kumaliza kabisa migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo hasa baada ya kubaini ofisi za wilaya na Mkoa wa Morogoro kushindwa kutatua mgogoro huku viongozi wake wakituhumiwa.

Waziri wa Ardhi alitaja kazi kubwa itakayofanya timu hiyo kuwa ni kupitia mashamba 15 yaliyofutwa na Rais sambamba na kufufua mipaka ya mashamba hayo na kazi hiyo itafanywa kwa na ushirikiano wa ngazi za wilaya.

"Tutayapitia mashamba yote yaliyofutwa na Rais na kujua kilichomo ndani yake na timu ya uhakiki niliyokuja nayo itanilitea mapendekezo ya namna ya kutumia mashamba na mengine watapewa wanaostahili na si kila mtu atapewa," alisema Lukuvi.

Alisisitiza kuwa wale wote waliojimilikisha mashamba yaliyofutwa na Rais watanyang'anywa na kupatiwa wanaostahili na mengine yatatolewa kwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa ajili ya kupatiwa wawekezaji.

Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mazingira katika Halmashauri ya Kilosa, Ibrahim Mndembo, alisema mashamba 25 yenye ukubwa wa ekari 23,596 kwenye maeneo ya Msowero, Magole na Chanzulu katika wilaya ya Kilosa yamebatilishwa umiliki baada ya wamiliki wake kushindwa kuyaendeleza.

Alisema kati ya mashamba hayo, 15 yalibatilishwa miliki zake katika kipindi cha uongozi wa serikali ya awamu ya tano.

Mashamba yenye mgogoro na wananchi katika wilaya ya Kilosa ni Noble Agriculture Enterprises, Magereza dhidi ya wananchi wa Mabane, Mbigiri na Mabwegere, Chadulu Estate, Shamba la Swai dhidi ya wananchi wa Ilonga na shamba la Mauzi Estate Malangali.

Habari Kubwa