Mauzo Soko la Hisa D`Salaam yashuka

21Sep 2016
Elizaberth Zaya
Nipashe
Mauzo Soko la Hisa D`Salaam yashuka

MAUZO katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), yameshuka kwa asilimia 81 kutoka Sh. bilioni 9 mpaka kufikia Sh. bilioni 1.7 kutokana na kushuka kwa idadi ya uuzaji wa hisa kufikia Sh. 340,000 kwa wiki hii.

Patrick Mususa akizungumza na waandishi wa Habari akielezea hali ya mauzo katika soko la hisa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mwandamizi wa Masoko wa DSE, Mary Kinabo, alisema kuwa mauzo hayo yameshuka kutokana na ukubwa wa mtaji wa soko kushuka kwa asilimia 2.79 kutoka Sh. trilioni 21.3 hadi kufikia Sh. trilioni 20.7.

Kinabo alisema kuwa ukubwa wa mtaji kutoka kampuni ya ndani umebaki kwenye kiwango kile kile cha Sh. trilioni 8.2 kutoka wiki iliyopita.

Alisema kuwa licha ya idadi ya mauzo kushuka, lakini pia benki ya CRDB imeshika nafasi ya kwanza katika kuuza na kununua hisa kwa asilimia 53 ikifuatiwa na kampuni ya Bia nchini (TBL) kwa asilimia 35 huku kampuni ya Swissport ikishika nafasi ya tatu ya kununua hisa kwa asilimia tatu.

Aliongeza kuwa licha ya viashiria vya soko kushuka kwa alama 36.6 baada ya bei za hisa kutoka TBL kushuka kwa asilimia 1.08, viashiria vya huduma za kibenki na kifedha vimepanda kwa alama 3.64 baada ya mauzo ya DSE kupanda kwa asilimia 11.5.

Habari Kubwa