Mavunde akuta zaidi ya wafanyakazi 300 hawana vifaa vya kujikinga

12Jan 2017
Ashton Balaigwa
Nipashe
Mavunde akuta zaidi ya wafanyakazi 300 hawana vifaa vya kujikinga

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Antony Mavunde, amefanya ziara ya kushtukiza katika kiwanda cha nguo cha 21Century na kukuta wafanyakazi zaidi ya 300 wakiwa hawana vifaa maalumu vya kujikinga wakati wa kufanya kazi.

NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Antony Mavunde.

Ziara hiyo ililenga kuzungumza na wafanyakazi na kusikiliza kero zinazowakabili na kuangalia kama wahusika wanazingatia sheria za usalama wa kazi.

Wafanyakazi hao walimueleza Naibu Waziri huyo kuwa wamekuwa wakilipwa mishahara midogo ambayo hailingani na saa wanazopangiwa kufanya kazi na pale wanapolalamika wanatishiwa kufukuzwa kazi.

Akizungumza mara baada ya kujionea hali hiyo ya wafanyakazi kutokuwa na vifaa vya kujikinga, Mavunde aliziagiza Mamlaka husika zinazosimamia sheria za kazi kuwachukulia hatua stahiki viongozi husika kwa kuwa sheria zinawataka kuzingatia miongozo ya kazi kwa wafanyakazi wao.

Kuhusu malalamiko ya mapunjo ya mishahara na kufanya kazi zaidi ya saa 12, aliagiza maofisa wa wizara hiyo kufanya uchunguzi wa kina ili kupata ukweli wa jambo hilo kama wawekezaji wanakiuka mikataba ya kazi.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri, amezindua utoaji wa mikopo yenye thamani ya Sh. milioni 26 kwa wajasiriamali 89 wa Kijiji cha Kiloka, Wilaya ya Morogoro, fedha ambazo zimetolewa na Mfuko wa Rais wa kujitegemea.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Mavunde, aliwataka vijana kuacha tabia ya kulalamika na badala yake wajishughulishe na ujasirimali ili kujiongezea kipato.

Aidha, aliwataka viongozi wa mfuko huo, kuendelea kutoa elimu kwa wahitaji ili uwafikie Watanzania wengi na kuondokana na umaskini.

Mapema, Mkurugenzi wa mfuko huo, Haighat Kitale, alisema mikopo hiyo inatolewa kwa riba ya asilimia 15 kwa wanawake na asilimia 12 kwa vijana, ikiwa na lengo la kusaidia kuwezesha vijana kujiajiri.

Habari Kubwa