Mawakala wataka 210 zirudishwe Bandari

14Feb 2016
Christina Mwakangale
Nipashe Jumapili
Mawakala wataka 210 zirudishwe Bandari

CHAMA cha Wakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), kimeitaka Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuziruhusu kampuni 210 za Mawakala wa Uondoshaji Mizigo Bandarini, kufanya kazi katika bandari hiyo, kwani kuzisitishia kufanya kazi kunaipotezea serikali mapato na kupoteza ajira za Watanzania wengi.

Waziri Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Prof.Makame Mbarawa

Hata hivyo, Taffa imesema kuwa saa chache kabla ya kuzungumza na waandishi jana, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof.

Makame Mbarawa amekubali ombi lao la kumtaka kuunda kamati ili kuchunguza sakata la malipo waliyoyafanya TPA, licha ya mamlaka hiyo kudai kuwa malipo hayakufanyika kwa baadhi ya kampuni hizo.

Rais wa Taffa, Stephen Ngatunga aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam kuelezea suala la kusitishwa kufanya kazi kampuni hizo tangu Februari 9 mwaka huu, kwa madai ya kuwa na ufanisi mdogo wa kazi, kushindwa kuwasilisha vielelezo vya malipo pamoja na nyaraka tofauti.

Alisema taarifa za kutolipwa ushuru si za kweli na kwamba tume hiyo ianze kuichunguza TPA pamoja na benki ambazo zilipokea malipo hayo.

“Sisi kama watendaji wakuu tunataka kuuthibitishia umma wa Watanzania, wabunge, serikali kwamba malipo tulifanya na vielelezo tunavyo, waulizwe TPA na benki ambazo hadi sasa hazijatoa ripoti kuhusu fedha hizo tangu sakata hili lianze,” alisema Ngatunga.

Alisema awali TPA ilizisitishia kampuni 48 kufanya kazi katika bandari hiyo na kisha zikafuata kampuni 83 na Februari 9 mwaka huu kampuni nyingine 210 zimesitishwa.

Alisema kufungiwa huko kunaikosesha serikali mapato kwani wageni wengi hivi sasa wanaopitisha mizigo katika bandari hiyo, wamehama na kupitisha mizigo katika bandari ya Mombasa nchini Kenya na Durban, Afrika Kusini.

Akizungumzia upande wa kamati itakayoundwa, Ngatunga alisema baadhi ya wajumbe watatoka Jeshi la Polisi, Usalama wa taifa na mmoja kutoka TAFFA.

“Majina ya wajumbe wa kamati hiyo yatafahamika hadi kufikia jioni ya leo (jana), na yatawekwa wazi na waziri ametuhakikishia kamati kuanza kazi mara moja,” alisema Ngatunga.

TPA ilizisitishia kampuni 210 kufanya kazi katika bandari hiyo, ambazo baadhi yake ni kampuni ya Bakhresa Food Products Ltd, Boston Forwarders Ltd, Babylon Freight Ltd, Beam Tanzania Ltd, Best Ocean Air Ltd, Break Through Holdings Ltd na Business Service Promotion Ltd.

Makampuni mengine ni Ujiji C & F Ltd, United Youth Shipping Co. Ltd, United family Co. Ltd, Uwanji General Traders Ltd, Uprising C & F Ltd, Upland Freight Ltd, Vigu Trading Ltd, Vamwe Investment Co. Ltd na Rungwe Trading Ltd.

Meneja Mawasiliano wa TPA, Janet Ruzangi aliiambia Nipashe kuwa mawakala hao walipewa taarifa kabla, ili wawasilishe vielelezo hivyo lakini hawakufanya hivyo.

“Tuliwapa taarifa kabla za kwamba watekeleze madai ambayo TPA iliwaagiza, lakini hawakufanya hivyo tumewafungia hadi watakapoleta vielelezo vya malipo mbalimbali wanayofanya na baadhi ya nyaraka, wakitimiza masharti yataendelea na kazi yao,” alisema Ruzangi.

Habari Kubwa