Mbaroni tuhuma mauaji kada wa Chadema

15Jun 2019
Idda Mushi
MOROGORO
Nipashe
Mbaroni tuhuma mauaji kada wa Chadema

JESHI la Polisi mkoani Morogoro linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya mkulima na Katibu Mwenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilaya ya Malinyi, Lucas Luhambalimo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa awali,  Luhambalimo (42) alikuwa na ugomvi na mkazi mmoja wa eneo hilo, Francis Kologaki, maarufu kama Mwanampalu wa kijiji cha Munga wilayani Malinyi, ambaye ni miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa kuhusika na mauaji hayo.

Mbali na Kologaki, watuhumiwa wengine ni Robson Mgeni na Memory Mbegalo, wote wakazi wa Mtimbira na kwamba uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha mauaji hayo  kulipiza kisasi kutokana na mgogoro wa mashamba.

Alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa kulikuwa na ugomvi baina ya watu hao na Septemba 3, mwaka jana, Luhambalimo alimshtaki Kogolaki kwa madai ya shambulio katika Mahakama ya Mwanzo Mtimbira. Katika kesi hiyo, Kagolaki alihukumiwa kwenda jela miezi mitatu au kulipa faini ya Sh. 50,000 na alilipa fedha hizo.

Baadaye Desemba 3, mwaka jana, Kogolaki na wenzake wawili walifunguliwa kesi ya madai katika Baraza la Ardhi la Kata, wakati huo Luhambalimo akiwa shahidi wa shauri hilo na ilitakiwa Juni 13, mwaka huu, afike barazani hapo kwa ajili ya kutoa ushahidi.

Hata hivyo, alisema siku ya tukio majira ya usiku wa manane, katika kijiji cha Munga, Luhambalimo ambaye alikuwa na wake wawili, Anastazia Sandi (42) na Zaituni  Matandiko (42), alikuwa amelala kwa mkewe (Zaituni). Ghafla alisikia vishindo vya watu wakitembea nje ya nyumba yao na alimwamsha mkewe na kumjulisha juu ya hali hiyo.

Kamanda Mutafungwa alisema Luhambalimo aliamua kuchungulia nje kupitia uwazi wa ukuta na kwa msaada wa mbalamwezi, aliwaona watu watatu na kumtambua Francis Kogolaki akiwa ni miongoni mwa watu hao.

Kutokana na hali hiyo, alimjulisha mkewe juu ya watu hao, ambao walizunguka upande mwingine wa nyumba na mwanamume huyo akawafuata upande huo tena kuchungulia, lakini ukasikika mlipuko mithili ya bunduki.

"Mwanaume yule (marehemu) akarudi kwa mkewe akiwa anavuja damu kichwani na akamweleza alipigwa na watu wale na mke alipochungulia tena nje kwenye uwazi, aliwaona watu wale watatu akiwamo mmoja aliyemtambua kuwa ni Francis wakiondoka eneo la nyumbani kwao," alisema Kamanda Mutafungwa.

Alisema baada ya tukio hilo, mwanamke huyo alipiga kelele za kuomba msaada na majirani walijitokeza na walipopewa taarifa kuhusu watu wale watatu walioonekana, walijaribu kuwafuatilia na kuwatafuta bila mafanikio, hivyo kumchukua  Luhambalimo na kumpeleka katika Kituo cha Afya cha Mtinmbira kwa ajili ya matibabu. Hata hivyo, alipoteza maisha akiwa njiani na wananchi wakafikisha taarifa katika kituo cha polisi.

"Polisi walipokwenda eneo la tukio walikuta kipande cha chuma chenye umbo la duara ambacho hutumika kwenye bunduki zinazotengenezwa kienyeji. Mwili  wa marehemu ulichukuliwa na baada ya uchunguzi ulikabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya maziko,” alisema.

Kamanda alisema kutokana na tukio hilo, polisi waliendesha msako mkali kwa kushirikiana na wananchi na hatimaye kuwakamata watuhumiwa. Watuhumiwa hao, alisema wote watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili.

Habari Kubwa