Mbegu bora madume ya ng’ombe yazaa matunda

07Sep 2021
Grace Mwakalinga
Rungwe
Nipashe
Mbegu bora madume ya ng’ombe yazaa matunda

UPATIKANAJI wa mbegu bora za madume ya ng'ombe kwa wafugaji wilayani Rungwe, mkoani Mbeya umechochea ongezeko kwa uzalishaji wa zao la maziwa kwa kuzalisha lita 200,000 kwa siku na kuingizwa sokoni.

Mwenyekiti wa Muungano wa Chama cha Wafugaji wilayani Rungwe (MUHAMARU), Asha Lukaja, alisema hayo kwenye elimu ya kutumia teknolojia za kisasa za ufugaji kwa kuwatumia maofisa ugani waliosambazwa wilayani humo na Kampuni ya Asasi kwa kushirikiana na Serikali ya Denmack nchini Tanzania kwa lengo ya kuwawezesha wafugaji kuzalisha maziwa kwa tija na kuingiza katika mnyororo wa thamani.

Alisema kabla ya elimu hiyo walikuwa wakikabiliwa na tatizo la masoko na mbegu bora, Kiwanda cha Maziwa cha Asasi kimewapatia madume ya mbegu bora za ng'ombe ambayo yamesaidia ongezeko la majike na kuchochea ongezeko la uzalishaji wa zao la maziwa.

“Licha ya ongezeko la uzalishaji wa maziwa na uwepo wa masoko ya uhakika bado tatizo kwa baadhi ya wafugaji kuingiza sokoni maziwa yasiyokuwa na ubora jambo linalochangia kuchafua na kutia doa maziwa yanayozalishwa wilayani Rungwe,” alisema Lukaja.

Miongoni mwa wafugaji wilayani Rungwe, Fadhili Mbilinyi, alisema kuwapo kwa kampuni za ununuzi wa maziwa wilayani Rungwe kumeleta tija wa wafugaji kuongeza uzalishaji na kufuga kisasa.

Alisema kwa sasa wanazalisha kiasi kikubwa cha maziwa na uhakika wa upatikanaji wa soko ndani na nje ya wilaya hiyo.
Ofisa Mifugo Wilaya ya Rungwe, Dk. Dennis Kamily, alisema wafugaji wengi hawapendi kuwatumia maofisa ugani kujifunza namna bora ya kuzalisha maziwa bila kutumia vyakula visivyo salama kwa ng’ombe.

Mkaguzi wa Maziwa Wilaya ya Rungwe, Henry Mokiwa, alisema asilimia 20 ya maziwa yanayozalishwa na wafugaji wilayani humo yanakosa ubora kutokana na baadhi ya wafugaji kuongeza maji.

"Ukamuaji wa maziwa kiholela kwa baadhi ya wafugaji kunachangia kuzalisha bakteria 500 hadi 1,000 kila baada ya saa tatu na kusababisha madhara kwa watumiaji na kushauri wafugaji kuwatumia maofisa ugani ili kuboresha sekta ya maziwa nchini," alisema Mokiwa.