Mbegu za kisasa zaanza kuzalishwa

22Apr 2018
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe Jumapili
Mbegu za kisasa zaanza kuzalishwa

WAKATI serikali ikijiwekeza kuhakikisha taifa linapata maendeleo kupitia uchumi wa viwanda, tayari Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Ari Ilonga, iliyopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro, imeanza mbegu za kisasa za mazao yaliyopewa kipaumbe kwaajili ya kuzalisha malighafi zitakazotumika katika viwanda.

Mbegu hizo zitaonyeshwa katika maonyesho ya Nanenane ya Mwalimu Nyerere yanayofanyika kila mwaka mjini hapa yanahusisha wakulima wa mikoa ya Kanda wa Mashariki ambayo ni   Morogoro, Pwani, Tanga na Dar es Salaam.

Akizungumza katika uzinduzi msimu wa vipando kwaajili ya maonyesho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo Kanda ya Mashariki kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga, Dk. Geofrey Mkamilo, alizitaja teknolojia za mazao yaliyopewa kipaumbele katika uchumi wa viwanda ambazo zitazalishwa malighafi ni pamoja na pamba, miwa, mahindi, mpunga, nazi, alizeti na jamii  ya kunde ambayo tayari yamefanyiwa utafiti wa kina .

Dk. Mkamilo alisema hatua ya kuzalisha teknolojia hizo na kuzionyesha kwa wakulima inatokana na   kuanza kukamilika kwa ujenzi wa viwanda vya kuzalisha sukari, pamba na jamii ya kunde ambavyo kwa sasa vipo mkoani Morogoro vinavyohitaji malighafi kutoka kwa wakulima.

“Tayari hivyo viwanda vipo katika hatua ya kukamilika, hivyo sisi kama watafiti wa kilimo tumeamua kuanza kuwandaa wakulima kwa kuwatafutia mbegu za kisasa za kilimo zilizofanyiwa utafiti wa kina ambazo zitazalisha  malighafi zinazohitajika  kwenye viwanda hivyo na tutaanza kuzionyesha katika maonyesho ya wakulima ya Nanenane, mwaka huu,” alisema.

Alivitaja  viwanda vilivyo katika hatua ya ujenzi kuwa ni cha kuchakata mazao jamii ya  kunde kilichopo Wilaya ya Morogoro, viwanda vya kuchakata pamba vilivyopo wilaya ya Mvomero, Ulanga na Kilosa na Kiwanda cha kutengeneza sukari cha Mkulazi kilichopo Kilosa na Ngerengere, wilaya ya Morogoro.

Akizungumzia zao la alizeti alisema tayari michakato mbalimbali ya kutengeneza viwanda vidogo vya kukamua mafuta hayo umekamilika katika wilaya za Kilosa, Gairo, Mvomero na Wilaya ya Kilombero na  zao hilo limepewa kipaumbele kwa kutafitiwa kupatikana kwa mbegu bora.

Alisema zao la mpunga nalo limefanyiwa utafiti wa kina na kuanza kuzalishwa kwa mbegu bora kutokana na mahitaji makubwa kwa wakulima wa wilaya za Mvomero, Kilombero, Malinyi na Kilosa baada ya kukamilika kwa viwanda vya kuchakata mpunga katika maeneo hayo.

Mtafiti wa mazao ya  kunde, James Mwaipyana, alisema mazao hayo yakiwamo kunde, mbaazi, choroko, maharage na dengu yataupata uhakika wa soko baada kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda hicho kilichopo wilaya ya Morogoro, lakini bado yanahitajika zaidi nchi za Ulaya kwaajili ya kutengenezwa kwa protini, vyakula vya binadamu na wanyama, na biskuti.

 

Habari Kubwa