Mbegu za kiume zazalishwa maabara kwa mara ya kwanza

22Sep 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mbegu za kiume zazalishwa maabara kwa mara ya kwanza

Hizi ni mbegu za kwanza za kiume kuzalishwa kwenye maabara? Timu moja ya watafiti ya Ufaransa inadai mafanikio yamekaribia kuwashawishi wenye kuhoji kwa kuchapisha kazi yao kwenye jarida linaloheshimika kitabibu

Lakini baadhi ya watafiti wanasema ushahidi uliotolewa bado upo chini kiasi ambacho kinahitajika kutoa tamko hilo kubwa na la kihistoria.

Katika utafiti huo wa miaka 20, watafiti wa Kifaransa wamesema wametengeneza mbegu za kiume za binadamu na panya, wakianzia na seli za makende ziitwazo 'spermatogonia'.

Watafiti wa Kijapani walitengeneza mbegu za kiume za panya mwaka 2011, kama ambavyo walimudu watafiti wa Kichina mapema mwaka huu, lakini timu hiyo ya Wafaransa ni ya kwanza kudai kutengeneza mbegu za binadamu ziitwazo kiitalamu spermatozoa. “Imebaki asilimia 20 ya utafiti,” anasema Philippe Durand wa Kallistem, kampuni iliyo jijini Lyon inayofanya utafiti huo.

Mwaka jana, Kallistem ilipata hakimiliki ya utaalamu huo, lakini hili lilishindwa kuwaondolea shaka wanasayansi wote. Sasa, kazi iliyofanywa kwenye mbegu za kiume za panya na binadamu imechapishwa kwenye jarida linaloheshimika kitaaluma la Biology of Reproduction (Biologia ya Uzazi).

Kallistem anasema lengo ni kusaidia wanaume ambao hawana uwezo wa kutoa mbegu za kiume kutokana na matibabu ya kansa ya utotoni, ambayo mara nyingi huharibu 'spermatogonia'. Kwa kuchukua na kugandisha sampuli zenye 'spermatogonia' kabla wavulana hawajaanza matibabu, utalaamu huu unaweza kutengeneza mbegu za kiume kutoka seli hizi katika siku za usoni wakati watakapoamua kuwa na watoto.

Kazi ya siku 72
Durand na washirika wake walijaribu kuonyesha matokeo ya wazo hilo kwa kutengeneza mbegu za kiume kwa kutumia tishu za makende ya panya wadogo kiasi cha kutosha kuwakilisha wavulana ambao watafaidika na utaalamu huo.

Na ili kupata matokeo kama hayo kwa kutumia seli za binadamu, Durand alichukua tishu zilizochangwa na watu wanaofanyiwa tiba mbadala ya homoni ambayo hufanya tishu za makende zisinyae kurudi katika kipindi kabla ya balehe.

Durand anasema baada ya homoni na tishu kuchanganywa kitaalamu huwekwa kwenye mtungi ambao umefungwa kikamilifu ili kuzuia seli zisitoke nje, kisha watagiti huzizamisha kwenye chombo kikubwa chenye mchanganyiko sahihi wa viini lishe, vitamini, homoni na vichochezi vya ukuzi ambavyo hunyonywa na seli na kuzizimua zikue, mchakato ambao huchukua siku 72. Baada ya hapo, mtungi huondolewa, sampuli kuyeyushwa – na mbegu za uzazi zilizokomaa hutolewa.

Ingawa utafiti umechukuliwa kuwa hatua moja zaidi kuelekea mafanikio, bado haujaweza kushawishi watafiti wengine. “Huu utafiti unatia moyo, lakini seli zinazozalishwa wala hazifanani na mbegu za kiume zilizo komaa au ambazo hazijakomaa, iwe kwa panya au binadamu,” anasema Jacob Hanna wa Chuo cha Sayansi cha Weizmann cha mjini Rehovot, Israel, ambacho ni sehemu ya timu nyingine inayojaribu kutengeneza mbegu za kiume kwenye maabara.
“Ingawa nadhani utafiti ni muhimu, madai ya kutengeneza viasili vya mbegu za kiume (spermatogenesis) nje ya mwili hayajathibitishwa bila kuacha shaka kwenye utafiti,” anasema.

Mbegu hizo ziwe halisi ama la, Kallistem ipo katika mazungumzo ya awali ya kufanya majaribio ya kitabibu na ANSM, bodi ambayo huhalalisha tiba nchini Ufaransa. Kama mabo yote yatakwenda vizuri na fedha za kutosha kupatikana, majaribio yanaweza kuanza ndani ya kama miaka minne, anasema Durand.

Habari Kubwa