Mbeya, Tabora, Singida kuunganishwa kwa lami

30Jul 2021
Nebart Msokwa
Chunya
Nipashe
Mbeya, Tabora, Singida kuunganishwa kwa lami

SERIKALI imepanga kujenga kilomita 58 za barabara inayounganisha Mbeya na mikoa ya Tabora na Singida kuanzia mji wa Makongolosi wilayani Chunya kwa kiwango cha lami katika mwaka wa fedha 2021/22.

Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka.

Mbunge wa Lupa, Masache Kasaka, alisema hayo alipokuwa anazungumza na wananchi wa mji wa Makongolosi kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani hapa.

Alisema kwa sasa barabara ya Chunya – Makongolosi yenye urefu wa Kilomita 39 imekamilika, hivyo katika bajeti iliyopitishwa na Bunge hivi karibuni, zimetengwa fedha kwa ajili ya kuendeleza barabara hiyo na kwamba itakuwa inajengwa kwa awamu tofauti.

Kasaka pia alisema kuna barabara mbalimbali ambazo zitaboreshwa na serikali ili kuwasaidia wananchi wa maeneo ya pembezoni mwa miji kusafiri na kusafirisha mazao bila vikwazo.

“Serikali imetoa Sh. bilioni moja kwa ajili ya uboreshaji wa barabara zinazohudumiwa na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) katika wilaya yetu, hivyo naamini kuwa barabara nyingi zitaboreshwa,” alisema Kasaka.

Pia alisema katika wilaya hiyo kuna vijiji 12 na vitongoji 14 ambavyo mpaka sasa havijafikiwa na umeme lakini akasema tayari makandarasi wanaendelea kusambaza nishati hiyo kwenye vijiji vyote.

Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha vijiji vyote nchini vinaunganishiwa nishati hiyo ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao ikiwamo uanzishwaji wa viwanda vidogo.

Habari Kubwa