Mbulu walia na vitambulisho vya wajasiriamali

15May 2019
Cynthia Mwilolezi
MANYARA
Nipashe
Mbulu walia na vitambulisho vya wajasiriamali

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Joseph Mandoo, amesema wamepoteza vyanzo vya mapato kwa kuwapo kwa vitambulisho vya wajasiriamali kwenye eneo hilo na kusababisha upungufu wa mapato ya halmashauri hiyo.

kitambulisho cha wajasiriamali.

Mandoo aliyasema hayo jana kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo cha robo mwaka kilichofanyika mjini Mbulu.

Alisema uwapo wa vitambulisho hivyo vya ujasiriamali umesababisha changamoto ya kupoteza vyanzo vyao vya mapato hasa kwenye minada na magulio mbalimbali vijijini.

Alisema hivi sasa hawana uwezo wa kukusanya mapato waliyokuwa wanakusanya kwa wajasiriamali hao zaidi ya kufanikisha vyanzo walivyobaki navyo katika halmashauri hiyo.

"Hata hivyo tunatakiwa kujipanga upya ili kuhakikisha tunakusanya mapato ya ndani tuliyonayo kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kutoa asilimia 10 kwenye mikopo ya wanawake, vijana na wenye ulemavu," alisema Mandoo.

Alisema vyanzo vya mapato vilivyopo chini ya halmashauri hiyo vinapaswa kusimamiwa kikamilifu ili makusanyo hayo yapelekwe kwenye miradi mbalimbali iliyopo katika kata na vijiji.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga, alisema hivi sasa wamejipanga kuhakikisha wanaendelea kukusanya vyanzo vya mapato vilivyopo ili malengo ya makusanyo yafikie.

Kamoga alisema kwa kushirikiana na madiwani pamoja na watumishi wa halmashauri hiyo watafikia lengo la kukusanya asilimia 80 ya makusanyo ya ndani kama walivyodhamiria.

"Ushirikiano mkubwa tulionao hivi sasa tuuendeleze ili kuhakikisha tunakusanya mapato ya halmashauri yetu ipasavyo na kwa moyo mmoja na nguvu moja kama tunavyoshirikiana kwenye mambo mengine," alisema.

Diwani wa Viti Maalum wa Tarafa ya Dongobesh, Emiliana Shishi (Chadema), alisema wanapaswa kubuni vyanzo vipya baada ya vingine kuchukuliwa kwenye vitambulisho vya wajasiriamali.

Shishi alisema baada ya vyanzo hivyo kuchukuliwa hawatakiwi kukata tamaa zaidi ya kusonga mbele ili kuhakikisha hawatetereki kwenye ukusanyaji wa mapato.

Habari Kubwa