Mbunge alia na bodi ya chai Rungwe

07Apr 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mbunge alia na bodi ya chai Rungwe

MBUNGE wa Viti Maalumu (Chadema), Sophia Mwakagenda, ameitaka serikali kuvunja bodi ya chai ya Wilaya ya Rungwe kwa sababu wananchi hawana imani na bodi hiyo.

Akiuliza swali la nyongeza bungeni jana, Mwakagenda alisema wawekezaji wameingizwa kwenye bodi hiyo ambao kimsingi wanajiwekea matakwa yao.

Alitolea mfano kuwa mmiliki wa Kiwanda cha Wakulima Tea Company (Watco) ambaye ni mwekezaji kutoka nje wakati Mohamed Enterprise ni mzawa na serikali imemwambia aombe kibali upya jambo ambalo alihoji kama serikali iko tayari kuivunja bodi hiyo.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha, akijibu swali hilo, alisema bei ya chai hupangwa kwa mkutano wa wadau na kanuni inaruhusu majadiliano kufanyika kati ya mkulima na mnunuzi.

Hata hivyo alisema kuhusu kuvunjwa kwa bodi ni vigumu kusema moja kwa moja bodi ivunjwe huku akiahidi kuambatana na mbunge huyo kuwatembelea wakulima hao.

Katika swali la msingi, Mbunge huyo alihoji ni kwa nini wakulima wa chai wilaya ya Rungwe wanalazimishwa kuuza majani mabichi ya chai kwa bei ndogo kuliko wakulima wa chai wa Wilaya za Njombe na Lushoto.

Ole Nasha alisema bei dira ya majani mabichi ya chai hupangwa katika mkutano mkuu wa wadau wa chai ambao ni wa kisheria na hufanyika kila mwaka kabla ya msimu kuanza.

Alisema kwa kuwa bei dira hupangwa na kukubaliwa na wadau wote, tofauti ya bei kati ya eneo moja na jingine hutokana na majadiliano kati ya wakulima na wenye viwanda kama ilivyoainishwa kwenye kanuni.

Alisema majadiliano hayo ndiyo yaliyosababisha wakulima wa Wilaya za Mufindi na Njombe kulipwa Sh. 250 kwa kilo wakati wale wa Lushoto, Muheza, Korogwe na Kagera walilipwa Sh. 230 ambayo ni bei elekezi .

“Kwa upande wa Wilaya ya Rungwe, bei ni kati ya Sh. 240 na 250 kwa kilo ambayo ni juu ya bei ekelezi. Tofauti ya bei kwa maeneo hayo inatokana na malipo ya pili.

Kwa mfano katika mwaka 2015/16, Kampuni ya Uniliver inayomiliki viwanda vya Kibwele, Kilima na Lugoda imelipa malipo ya pili kati ya Sh. 80 hadi 200 kwa kilo,” alisema.

Alisema Kiwanda cha Watco cha Rungwe hulipa malipo ya kwanza Sh. 240 na ya pili ya Sh. 29 na kufanya jumla kuwa Sh. 269.

Hata hivyo alisema katika mwaka 2016/17 kiwanda cha Kibwele kinachomilikiwa na Uniliver kitatoa malipo ya pili ya Sh. 3 na jumla kuwa Sh. 253 na viwanda vya Kilima na Lugoda malipo yatakuwa kati ya Sh.100 na 200.

Habari Kubwa