Mbunge ashauri leseni 201 za madini kufutwa

12Jan 2021
Elisante John
Njombe
Nipashe
Mbunge ashauri leseni 201 za madini kufutwa

MBUNGE wa Jimbo la Ludewa mkoani Njombe, Joseph Kamonga, ameshauri serikali kufuta leseni 201 za wamiliki wa vitalu vya madini wilayani Ludewa ambao hawafanyii kazi maeneo hayo.

Ushauri huo aliutoa mwishoni mwa wiki kwenye kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Njombe (RCC), baada ya kupata taarifa kutoka kwa Kaimu Ofisa Madini, Fredrick Jirenga, kuwa wilaya hiyo ina jumla ya leseni 201 za umiliki wa maeneo ya madini, lakini kati ya hizo zinazofanya kazi ni tano pekee.

“Naishukuru ofisi ya madini Mkoa wa Njombe kwa kuweka data hizi hadharani, zamani haikuwa hivi tumeambiwa Wilaya ya Ludewa zipo leseni za madini 201, lakini zinazofanya kazi ni tano pekee, nashauri leseni hizi zifutwe bila kujali mmiliki ni nani ili kutoa nafasi kwa wachimbaji wadogo wenye uwezo wa kuyafanyia kazi maeneo hayo,” alisema Kamonga.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Andrea Tsere, alisema kuna maeneo yapo nje ya miradi ya Liganga na mchuchuma wilayani humo ambayo yalipaswa kumilikiwa na wachimbaji wadogo, lakini yamechukuliwa na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na kuwanyima fursa wachimbaji hao jambo ambalo linapaswa kutazamwa ili shirika hilo liwaachie na kutoa fursa kwa wachimbaji wadogo.

“Katika miradi ya chuma na makaa ya mawe wilayani Ludewa kuna maeneo yapo nje ya mradi hii, lakini yapo chini ya NDC, ombi langu hawa NDC wayaachie ili wapewe wachimbaji wadogo ambao wanauhitaji wa kufanya kazi na kutoa fursa kwao na serikali,” alisema Tsere...soma zaidi kupitia https://epaper.ippmedia.com

 

Habari Kubwa