Mbunge ataka mikakati kuvutia uwekezaji nchini

13May 2022
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Mbunge ataka mikakati kuvutia uwekezaji nchini

MBUNGE wa Kinondoni, Tarimba Abbas, ameitaka serikali kuweka mifumo rafiki ya kurahisisha ufanyaji wa biashara ili kuvutia zaidi uwekezaji nchini.

MBUNGE wa Kinondoni, Tarimba Abbas.

Akiuliza maswali bungeni jana, mbunge huyo alisema utekelezaji wa mifumo rafiki unasuasua huku akisema andiko la blue print (uchumi wa bluu) linaelekeza kutakuwa na mchanganuo wa jinsi ya kutekeleza na muda maalum.

“Je, serikali ipo tayari kuleta bungeni mchanganuo wa jinsi gani changamoto zake zinakwenda kutekelezwa na muda uliopangwa?” alihoji.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, alisema utekelezaji wa blue print ulianza mwaka 2018 na bado kuna vikwazo vichache na kwamba kuna umuhimu wa kuhuisha.

“Na wabunge watapata kujua utekelezaji wake na muda uliopangwa,” alisema na kubainisha kuwa hivi karibuni wizara itakuwa na vitengo kwenye halmashauri na kutakuwa na maofisa uwekezaji na biashara watakaoshirikiana na mamlaka ili kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini.

Alisema serikali imeendelea kufanya maboresho ikiwa ni pamoja na kurekebisha sheria, kuweka mifumo ya kielektroniki, kufuta au kupunguza tozo na ada kero.

“Nyingine ni kuanzisha vituo vya pamoja vya kutoa huduma, kusogeza huduma karibu na watumiaji, kuboresha mifumo ya ukaguzi wa pamoja, kuweka utaratibu wa ukaguzi unaozingatia vihatarishi, kujenga uwezo katika mamlaka za uthibiti na kuweka taratibu na kanuni za kujidhibiti,” alisema.

Habari Kubwa