Mbunge ataka soko la kisasa la wavuvi Ukanda wa Pwani

24Jun 2022
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Mbunge ataka soko la kisasa la wavuvi Ukanda wa Pwani

MBUNGE wa Viti Maalum (CCM), Mwantumu Zodo, amehoji lini serikali itajenga soko la kisasa la wavuvi kwenye Ukanda wa Pwani.

Akijibu swali hilo jana bungeni jijini hapa, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alisema serikali inaendelea kuboresha na kujenga masoko ya mazao ya uvuvi katika maeneo mbalimbali nchini, ukiwamo Ukanda wa Pwani.

Alisema kwa sasa serikali inaendelea na ujenzi wa soko la samaki katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kwa gharama ya Sh. bilioni 2.8.

“Awamu ya kwanza ya ujenzi huo tayari imeanza mwezi Februari, 2022 ambapo gharama iliyotumika hadi sasa ni Sh. bilioni 1.6,” alisema.

Aliongeza kuwa masoko yaliyopangwa kujengwa katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi kwa mwaka 2022/23 ni pamoja na Soko la Samaki la Kipumbwi wilayani Pangani.

“Soko litakalogharimu Sh. bilioni 1.24 ambapo soko hilo litaambatana na ujenzi wa chumba cha ubaridi chenye uwezo wa kuhifadhi tani 40 za samaki na kusimika mtambo barafu kwa gharama ya Sh. milioni 259.1,” alisema.

Vilevile, alisema kupitia programu maalum ya uchumi wa buluu na programu ya mkopo wa masharti nafuu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF), serikali imepanga kujenga masoko mapya katika maeneo ya Somanga na Kilwa Kivinje.

Habari Kubwa