Mbunge ataka wauza pombe kwenye viroba wapewe muda

07Mar 2017
Asraji Mvungi
ARUSHA
Nipashe
Mbunge ataka wauza pombe kwenye viroba wapewe muda

UTEKELEZAJI wa agizo la serikali la kudhibiti matumizi ya pombe zinazofungashwa kwenye ujazo mdogo maarufu kama viroba huenda ukawa mgumu katika Wilaya ya Monduli, baada ya baadhi ya viongozi na watendaji kugawanyika.

Kundi moja kati ya hayo linataka wananchi waliowekeza mitaji yao kwenye biashara hiyo waongezewe muda ili waepuke hasara isiyo ya lazima na lingine likipinga kwa madai kuwa muda wa kujadili suala hilo umekwisha.

Mgwanyiko na mvutano huo ulitokea katika kikao cha watendaji wa halmashauri hiyo na Naibu Waziri wa Tamisemi, Suleimani

Jafo, ukimhusisha Mbunge wa jimbo hilo, Julius Kalanga, ambaye alisema lengo lake sio kutetea maovu bali ni kuwaepushia wananchi hasara isiyo ya lazima kwa kuwa wengi wamekopa na wamelipa kodi zote za serikali.

Hata hivyo, madai hayo yalipingwa na Katibu Tawala wa wilaya hiyo, ambaye alisema hatua ya mbunge kujaribu kutetea suala hilo ni sawa na kutetea uovu.

Hizi pombe zimekuwa na athari kubwa kwa jamii, tumepoteza nguvu kazi kubwa ya vijana halafu bado unawatetea, kiukweli hili halikubaliki na ninasema mimi kama mtendaji mkuu katika wilaya hii nitalisimamia kwa nguvu zangu zote," alisema.

Akizungumza baada ya baadhi ya viongozi akiwamo mwenyekiti wa halmashauri hiyo kutumia busara kunusuru kikao hicho kisivunjike, Jafo alisisitiza umuhimu wa viongozi kuweka pembe ni tofauti zao na kushirikiana kwa maslahi ya wananchi.

"Kumbukeni wananchi wa Tanzania wanataka mabadiliko, na wakati Rais John Magufuli, anaingia madarakani aliwahakikishia wananchi kuwa ataongoza mabadiliko hayo kupitia ilani ya CCM," alisema.

Pamoja na serikali kupiga marufuku uuzaji wa pombe kwenye viroba wafanyabiashara wengi wa bidhaa hizo wamekuwa wakilalamika kuwa bado wana bidhaa nyingi zilizoko sokoni ambazo hazijanunuliwa hatua inayowasababishia hasara kubwa ikiwamo ya kushindwa kurudisha mikopo.

Habari Kubwa