Mbunge: Wakulima msiuze pamba yenu kwa walanguzi

17Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Mbunge: Wakulima msiuze pamba yenu kwa walanguzi

MBUNGE wa Geita Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu, amewashauri wakulima wa pamba wawe wavumilivu badala ya kuuza pamba hiyo kwa walanguzi kwa bei ya chini, huku serikali ikiendelea kuwatafutia soko zuri.

MBUNGE wa Geita Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu.

Amesema serikali ilishaahidi kuwa kama pamba hiyo haitanunuliwa kwa bei elekezi ya kilo moja kwa shilingi 800 hadi Agosti mwaka huu, serikali itainunua pamba hiyo ili kuwafidia wakulima hao.

Hatua hiyo imetokana na wafanyabiashara wengi kushindwa kununua kwa bei hiyo kutokana na bei ya soko la pamba duniani kuporoka.

Akizungumza kwenye mkutano uliofanyika katika eneo la Kasamwa mkoani Geita, Kanyasu alisema wafanyabiashara wameshindwa kukopa pesa benki kwa ajili ya kuinunua pamba hiyo kutokana na kukosekana kwa soko la kuiuza.

Kanyasu alisema kufuatia hali hiyo, baadhi ya wakulima wamekuwa wakiiuza pamba hiyo kwa shilingi 500 kwa kilo moja kwa walanguzi hali, inayowadidimiza kiuchumi.

Alitaja mikakati ambayo serikali imeshaichukua ikiwamo kuzungumza na Serikali ya Vietnam ambao tayari wameonyesha nia ya kununua pamba hiyo kwa wakulima.

Aidha, Kanyasu aliwaeleza wakulima hao kuwa Waziri wa Kilimo anatambua tatizo hilo na aliahidi kutembelea mkoa huo kwa ajili ya kuzungumza na wakulima hao.

Naye Juma Kaludushi, mkulima wa zao la pamba, alisema wakulima wengi akiwamo na yeye wamekuwa wakiuza pamba hiyo kwa walanguzi kwa bei ya chini kwa hofu kuwa pamba hiyo itaharibikia mikononi mwao.

"Pamba ipo majumbani mwetu muda unakwenda bora tuuze tu kwa walanguzi ili isiharibike kuliko tukapata hasara kabisa,” alisema mkulima huyo.

Kwa upande wake, Ester Nalamo, mkulima wa pamba alisema amelazimika kuuza pamba kwa bei ya chini ili aweze kuwalipia ada watoto wake kwa vile hana chanzo kingine cha mapato zaidi ya kuuza pamba.

Habari Kubwa