Mchakato wa mbinu kuvutia utalii

23Oct 2019
Godfrey Mushi
Same
Nipashe
Mchakato wa mbinu kuvutia utalii

SERIKALI imeanza mchakato wa kutafuta mbinu mbadala za kuvutia sekta ya utalii hasa katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi na Msitu wa Hifadhi ya Asili wa Chome maarufu kama Shengena, baada ya kuita watu wa utamaduni na sanaa kutunga nyimbo za hamasa ili kuvutia utalii wa ndani.

Katika taarifa yake jana, Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule, alisema uamuzi huo unalenga kuinua mapato ya hifadhi hizo na kuongeza idadi ya watalii au Watanzania wanaozitembelea kila mwaka.

"Tumetoa hadidu za rejea kuhusu aina ya nyimbo tunazozitaka kwamba ni lazima ziwe na maudhui ya utalii na mvuto wake uguse hisia za wasikilizaji au watazamaji wa mikanda ya video," alisema.

Pia, serikali imetoa mwongozo kama huo pia wa kutungwa kwa nyimbo za kuhamasisha uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, mwaka huu.

Zimo pia nyimbo za kuhamasisha uwekezaji katika sekta mbalimbali, afya ya uzazi salama, kupiga vita mimba za utotoni, ukeketaji, ukatili wa kijinsia na umuhimu wa kuvutia watoto wa jamii za wafugaji kuandikishwa darasa la kwanza kupata elimu ya msingi.

Nyimbo zinazotakiwa kutungwa zinatakiwa kuwa katika miondoko ya muziki wa kizazi kipya maarufu kama bongo fleva, dansi, ngoma za asili au nyimbo zenye mahadhi ya dini.

Hivi karibuni, mfanyabiashara wa sekta ya usafirishaji mkoani Kilimanjaro, Hussein Abdallah maarufu kama Kilenga, alianza kazi maalum ya kuvitangaza vivutio vya utalii vya Wilaya ya Same.

Wilaya hiyo ina vivutio adimu vya utalii katika kilele cha Msitu wa Hifadhi wa Shengena, vivutio vya asili na maisha halisi ya ndege aina ya tai na faru weusi ambao hawapatikani katika mbuga nyingine za Tanzania wanaoishi katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.

Alipoulizwa dhamira yake ni ipi katika suala la utalii, Kilenga alisema: “Dhumuni kubwa la kuanzisha kikundi changu cha Lukungu Sanaa Group ni kuhakikisha naitangaza vyema Wilaya ya Same pamoja na vivutio mbalimbali vilivyopo, kuelimisha, kuburudisha, uhamasishaji utunzaji mazingira na kuuenzi utamaduni wa kabila la Kipare."

Katika kutekeleza adhima ya kuvutia utalii, Mkuu wa Wilaya hiyo, Senyamule, alitangaza kuwa ofisi yake itaitisha kongamamano la wadau wa utalii, kujadili namna bora ya kuchochea hamasa itakayovutia wageni kutoka nchi mbalimbali duniani kuitembelea Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi na Msitu wa Hifadhi wa Shengena.

Habari Kubwa