Mfumo stakabadhi ghalani kuboreshwa

07Sep 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Mfumo stakabadhi ghalani kuboreshwa

SERIKALI imeahidi kufanya maboresho ya kero zinazojitokeza kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani ikiwamo kufanya mapitio kwenye sheria na kanuni ili uwe na tija kwa wakulima nchini.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, aliyasema hayo katika semina iliyotolewa na wizara hiyo kwa wabunge kutoka kamati tano za Bunge kuhusu utekelezaji wa mfumo huo.
 
Kamati hizo ni ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, Kamati ya Bajeti pamoja na Kamati ya Hesabu za Serikali.
 
Akizungumza kwenye semina hiyo, Kigahe alisema mfumo huo unasaidia kuweka bei shindani yenye tija kwa wakulima.
 
“Serikali ina mikakati ya kutatua changamoto ambazo zimejitokeza katika kutekeleza mfumo huu ikiwa ni pamoja na kuboresha kujenga maghala mengi ili kupunguza changamoto za wakulima wadogo kupeleka maghala ya umbali hivyo tuendelee kujenga maghala mengi ili kuhifadhi mazao yetu na kupata bei nzuri," alisema.
 
Alisema pia serikali inaendelea kusajili maghala na kukaribisha wadau kujenga kwa kuwa ni biashara nzuri ili kusaidia kuhifadhi mazao na kuuza kwa bei nzuri.
 
Hata hivyo, alisema wameweka wakaguzi ili kudhibiti ujanja ujanja unaofanywa wa kuwapunja wakulima.
 
“Pia kukagua ubora kabla ya kuhifadhi ghalani kama Mbunge Kunti alivyoshauri kukagua ubora ili kuhakikisha bidhaa unayolipwa iwe halali na haijachanganywa na vitu,” alisema.
 
Kadhalika, alitoa wito kwa wabunge wa Kanda ya Ziwa kuanza kutoa elimu kwa wananchi kulima kilimo biashara kwa kuwa mazao ya choroko na dengu yana soko na kuahidi serikali itatoa elimu kwa kanda hiyo.
 
Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Asangye Bangu, alisema dhumuni la kuanzishwa mfumo huo ni kukuza juhudi za serikali kurasimisha mifumo ya masoko iliyopo ili kupunguza vipingamizi mbalimbali vinavyokwaza uzalishaji wenye tija.
 
Bangu amesema mfumo huu una manufaa mbalimbali ikiwamo kuwapa nguvu wawe kamili hususani wakulima kupigania bei nzuri katika soko kwa kuhamasisha kutumia mfumo wa pamoja kukusanya na kuuza, kutoa uhakika wa ubora na bidhaa na Mfumo wa uthibitisho, kupunguza mashaka na gharama za ushughulikiaji kwa wafanyabiashara wa bidhaa na wakulima wakati wa kufanya biashara.
 
Alisema mfumo huo umesaidia  kuweka utaratibu wa kupata taarifa na takwimu za soko na mauzo za kuaminika kwa wadau mbalimbali,  kuongeza ushiriki wa wafanyabiashara wa bidhaa wenyeji katika biashara ya kimataifa, kuhimiza usindikaji nchini wa mazao ya msingi kwa lengo la kuongeza thamani nakukuza uendelezaji wa viwanda.
 
Naye Mrajisi Mkuu wa Tume ya Vyama vya Ushirika nchini, Dk. Benson Ndiege, alisema mfumo huo ukiimarishwa utakuwa mkombozi wa mkulima na kwamba Tume hiyo imeshaanza mchakato wa kukusanya maoni na kurekebisha Sheria ya Ushirika.