Mganda alivyochangamkia fursa msiba wa Dk. Mengi

11May 2019
Salome Kitomari
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mganda alivyochangamkia fursa msiba wa Dk. Mengi

RAIA wa Uganda, Molakya Geofrey, juzi alichangamkia fursa ya biashara ya kuuza vifaa vya kuwekea funguo, baji za picha ya aliyekuwa  Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Marehemu Dk. Reginald Mengi.

Mganda huyo ambaye alionekana akiuza vitu hivyo kwa Sh. 1,000 kwa watu waliokuwa kwenye mistari ya kwenda kuaga mwili wa Dk. Mengi katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Moshi Mjini.

“Baada ya kusikia taarifa za kifo cha mpendwa wetu Dk. Mengi, niliingia kwenye Facebook na kubaini watu wengi wanampenda (Dk. Mengi) sana. Kama raia wa Uganda niliona ni fursa na kutengeneza vifaa vya kuwekea funguo na baji za kuvaa shingoni,” alisema.

Alisema upendo anaoweza kuuonyesha kwa Dk. Mengi ni kuchangamkia fursa ya kujipatia kipato kwa ajili ya maisha yake, na kwamba hivi karibuni atatengeneza kalenda atakazoziuza nchi mbalimbali.

“Nimeonyesha upendo wa hali ya juu kwa kuwa nimetoka Uganda nikapitia Kenya na sasa nipo Tanzania, nauza vitu hivi ambavyo vinanipatia kipato, nafanya utalii, lakini nafanya kitu cha upendo kwa mtu aliyependwa na Watanzania,” alisema.

Alisema baada ya kuona mapokezi ya Mwenyekiti kuanzia Uwanja wa Ndege wa KImataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na kutembezwa kwenye bararabara mbalimbali na baadaye siku ya kuaga na kupokelewa mkoani Kilimanjaro, aliona ni fursa kubwa na muhimu kwake.

Vifaa hivyo vilikuwa na picha mbalimbali za Dk. Mengi ikiwamo ambazo yuko na familia yake, na alikuwa na kijana anayemsaidia kuuza, huku akiwa amehifadhi kwenye begi jeusi alilobeba mgongoni.

Aidha, wananchi waliokuwa kwenye mstari walionekana kuchangamkia bidhaa hizo kwa kila mmoja kutaka kuvaa baji yenye picha ya Dk. Mengi.

Dk. Mengi alifariki dunia Mei 2, mwaka huu Dubai katika Falme za Kiarabu, na mwili wake ulisafirishwa Mei 6, mwaka huu, na kupokelewa JNIA kisha uliagwa katika viwanja wa Karemjee jijini Dar es Salaam Jumanne.

Mwili huo ulisafirishwa Jumatano hadi mkoani Kilimanjaro na kupokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), na baadaye kupelekwa Machame ambako ulilala kwa usiku mmoja na kufanyiwa ibada katikwa Usharika wa Moshi mjini.

Mwili wa Dk. Mengi ulizikwa Mei 9, mwaka huu, katika makaburi ya familia katika kijiji cha Kisereni Kata ya Machame, Wilaya ya Hai.

Habari Kubwa