Mghwira ataja dawa migogoro

20Jul 2019
Mary Mosha
MOSHI
Nipashe
Mghwira ataja dawa migogoro

MKUU wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, amewataka wananchi wanaoishi katika vijiji vya Mtakuja na Mserikia katika Wilaya ya Moshi kuanza kupunguza idadi ya mifugo kwa kuuza ikiwa ni njia mojawapo ya kukabiliana na migogoro ya kugombea maeneo ya malisho kati ya wafugaji na wakulima.

MKUU wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira.

Alisema kuna haja ya jamii hiyo kuanza kufuga kisasa na kupunguza idadi ya makundi makubwa ya mifugo ambayo yamekuwa yakiharibu mashamba ya wakulima na kusababisha migogoro ya mara kwa mara.Alitoa agizo hilo juzi, wakati akizungumza na wananchi wa vijiji juu ya njia bora za kumaliza migogoro kati ya makundi hayo mawili.

“Viongozi wa vijiji hivi viwili, nataka muandae mpango mkakati wa kuisaidia jamii ya wafugaji kuwa na shughuli mbadala za kuwaingizia kipato, “alisema na kuongeza:

”Aidha naagiza na ninyi wafugaji fikirieni kupunguza sehemu ya mifugo yenu na kubakisha idadi ndogo ya mifugo kwa sababu ongezeko la watu limesababisha ardhi kuwa finyu na haitoshi kwa malisho na kilimo.”Baada ya kauli hiyo, baadhi ya jamii ya wafugaji katika eneo la Mserikia akiwamo Lomayani Alaisi, alisema hawana tatizo na agizohilo kwa kuwa wanafahamu linalenga kuwahimiza kufuga kisasa na kuepukana na migogoro isiyo ya lazima.“Mimi binafsi sina tatizo na nitatii agizo la serikali la kutaka kupunguza mifugo na kuanza kufuga mifugo ya kisasa, naijua adha kubwa ninayoipata kipindi cha kiangazi tunapohama na makundi ya mifugo kwa ajili ya kuitafuta malisho katika mikoa ya jirani. Kazi kubwa iko kwa wenzangu kukubaliana na jambo hili ambalo kwao ni gumu,” alisema LomayaniDiwani wa Mabogini (Chadema), Emmanuel Mzava, akizungumza mbele ya mkuu huyo wa mkoa, alisema wameanza utaratibu wa kutenga maeneo ambayo hayajaendelezwa kwa ajili ya malisho.