Mgodi wafadhili wajasiriamali

25Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Kasulu
Nipashe
Mgodi wafadhili wajasiriamali

WAWAKILISHI wa vikundi vya wajasiriamali kutoka vijiji vinayozunguka Mgodi wa Dhahabu wa Barrick Bulyanhulu ulioko katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga, wanashiriki maonyesho ya tatu ya wajasiriamali kitaifa yanayoendelea wilayani Kasulu kwa ufadhili wa kampuni hiyo.

Maonyesho hayo ambayo yatafikia tamati Septemba 30, mwaka huu, yakiwakutanisha wajasiriamali kutoka maeneo mbalimbali nchini, yameandaliwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma na yalizinduliwa rasmi na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango.

Lengo la maonyesho hayo ni kutoa fursa ya kupanua wigo wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa na viwanda vidogo, kubadilishana ujuzi na uzoefu kwa wanajisiriamali na wanaviwanda pamoja na kuonyesha teknolojia mbalimbali zinazozalishwa nchini.

Akizungumza kwa niaba ya wajasiriamali wenzake waliowezeshwa na Barrick kushiriki katika maonyesho hayo, Clementina Felix, anayejishughulisha na ushonaji na ubunifu wa mavazi, aliishukuru Barrick Bulyanhulu kwa kuwawezesha kushiriki maonyesho hayo makubwa ambayo yatawawezesha kujifunza mambo mbalimbali ili kukuza biashara zao.

"Kupitia maonyesho haya tutaweza kupata fursa ya kuonyesha bidhaa tunazozalisha, pia tutaweza kupata elimu ya kufungasha bidhaa, urasimishaji biashara na kufungua fursa zaidi za masoko, tumekuja na bidhaa zaidi ya 100 za kuonyesha,” alisema Felix.

Aliongeza kuwa miongoni mwa wajasiriamali waliowezeshwa na Barrick, wanajihusisha na kilimo cha mazao ya nafaka, mboga na matunda, wafugaji wa kuku na nyuki,  washonaji wa nguo na watengenezaji wa mazulia na viatu.

Ofisa Uhusiano na Jamii wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Antony Sebastian, alisema wajasiriamali hao ni sehemu ya shughuli za maendeleo ya Mgodi wa Bulyanhulu ambao wanawezeshwa kupewa elimu ya ujasiriamali na kwa wale wanaojishughulisha na kilimo wanapatiwa mbegu, mbolea na dawa za kuulia wadudu ili wafanikiwe kuendesha kilimo cha kibiashara.

Sebastian aliishukuru SIDO kwa kuandaa maonyesho hayo yaliyowakutanisha wajasiriamali na wadau mbalimbali wa sekta ya ukuzaji wa biashara ndogo.

Habari Kubwa