Mgombea aahidi soko la uhakika wakulima pareto

16Oct 2020
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Mgombea aahidi soko la uhakika wakulima pareto

MGOMBEA ubunge wa Mbeya Vijijini (CHADEMA), Joseph Mwasote, maarufu China wa China, amesema akichaguliwa kuliwakilisha jimbo hilo bungeni, atahakikisha anawasaidia wakulima wa pareto kupata soko la uhakika.

Alitoa ahadi hiyo juzi katika mkutano wa kampeni Kata ya Ilembo, akisisitiza kuwa kwa sasa zao hilo halina soko la uhakika.

Mwasote alisema baadhi ya wakulima wameanza kukata tamaa na kuacha kulima zao hilo na badala yake wameanza kupanda miti ya mbao pamoja na mazao mengine yakiwamo mahindi na viazi mviringo ambayo ni maarufu kwenye ukanda huo.

Alisema akichaguliwa na wananchi hao, atahakikisha anashirikiana na serikali kutafuta wawekezaji ambao watawekeza viwanda vya kuchakata zao hilo kwenye ukanda wa Umalila ambao zao hilo linazalishwa zaidi ili kuwasogezea soko wananchi.

“Sisi huku ndiyo wakulima wakubwa wa pareto na tunazalisha pareto yenye sumu nyingi, lakini kiwanda kimeenda kuwekwa Mafinga mkoani Iringa na wanunuzi wanapeleka huko, jambo ambalo halitusaidii sisi huku, hivyo ninaombeni kura zenu ili nikapambanie suala hilo,” alisema Mwasote.

Alisema mbali na zao hilo, wakulima wa viazi mviringo pia wanakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa soko la uhakika wa zao hilo kutokana na miundombinu ya barabara kutokuwa rafiki na hivyo akawaahidi wananchi hao kuwachagua wagombea wa CHADEMA.

Alisema serikali ya chama hicho itaboresha miundombinu ya barabara kwenye maeneo yote ya uzalishaji ili kuwarahisishia wananchi usafirishaji wa mazao kutoka kwenye mashamba kwenda kwenye masoko.

Alisema baadhi ya wanunuzi wa zao hilo huwa wanaishia katika Mji wa Mbalizi hasa kipindi cha mvua wakiepuka kuongezeka kwa gharama endapo magari yao yatakwama kwenye maeneo ya vijijini ambako ndiko zao hilo linalimwa.

Mgombea huyo alisema kwenye Ilani ya CHADEMA, kuna utaratibu wa kuruhusu wakulima kuuza mazao yao mahali popote wanapoona wao kuna soko na kwamba ambao hawatakuwa na uwezo wa kusafirisha, watawezeshwa kuyafikia masoko hayo.

Habari Kubwa