Mgomo wasababisha ukosefu wa nyama

03Sep 2017
Renatha Msungu
Nipashe Jumapili
Mgomo wasababisha ukosefu wa nyama

MGOMO wa kampuni ya kuchinja ng'ombe mkoani Dodoma ya Tanzania Meat Co. Ltd, umezua taharuki ya aina yake baada ya kitoweo hicho kuadimika kwa walaji.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe ulibaini kuwa taharuki hiyo ilizidi kuongezeka baada ya bei kupanda maradufu katika baadhi ya mabucha yaliyokuwa na akiba ya nyama ya siku kadhaa nyuma, hivyo kuathiri pia biashara katika maeneo ya kuuzia vyakula na nyama choma.

Taarifa kuhusiana na mgomo huo zilieleza kuwa chanzo chake ni kuongezeka kwa gharama za uchinjaji hadi Sh. 23,600 kutoka 20,000, kiasi ambacho wafanyabiashara wa nyama waligoma kulipa, hivyo kusababisha uhaba wa bidhaa hiyo.

Akizungumza na Nipashe jana, Kaimu Meneja wa kampuni hiyo, Nashoni Kalinga, alisema wamelazimika kuongeza gharama ya uchinjaji baada ya kusajiliwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) na kutakiwa kuongeza asilimia 18, ambazo ni sawa na kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Kalinga alisema  mpaka sasa hakuna uchinjaji wowote unaoendelea kwa sababu hawawezi kupunguza kiasi hicho cha kodi ambacho kipo kisheria

Katibu wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Nyama Dodoma (UWAWABUDO), Swalehe Said, alisema ongezeko hilo kwao limewafikia ghafla na ndiyo maana wamegoma kutoa kiasi hicho cha fedha

Habari Kubwa