Mhadhiri UDSM afichua ushiriki mdogo wanawake kwenye siasa

19Jul 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Mhadhiri UDSM afichua ushiriki mdogo wanawake kwenye siasa

MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Consolata Sulley, amesema licha ya nchi kusaini mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda na kubadili sheria na kanuni, lakini bado kuna ushiriki mdogo wa wanawake kwenye siasa.

RAIS JOHN MAGUFULI AKIHUTUBIA

Dk. Sulley aliyasema hayo katika mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) wakati akiwasilisha mada ya jinsia na uwezeshaji wa wanawake katika masuala ya siasa.

Alisema bado kuna changamoto ya wanawake kushiriki kwenye siasa na uongozi ikilinganishwa na wanaume.

“Wanawake wengi ni wapiga kura wazuri ukiangalia takwimu za wapiga kura tupo wengi. Takwimu za mwaka 2015 zinaonyesha wanawake walioandikishwa kupiga kura walikuwa ni asilimia 53, waliotia nia walikuwa asilimia 28.7, waliogombea walikuwa asilimia 19, walioshinda ubunge asilimia 9.5 na waliochaguliwa kuwa madiwani ni asilimia 5.2,” alisema.

Alisema kwa takwimu hizo wanawake waliojiandikisha kupiga kura walikuwa wengi, lakini waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa kisiasa asilimia zilishuka.

Ofisa wa Programu wa TCD, Lucy Agustino, alisema kupitia mradi uliofadhiliwa na UN Women, wamelenga kuongeza idadi ya ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi uchaguzi ujazo.

“Ipo mikakati tuliyojiwekea, moja wapo ni viongozi wa vyama vya siasa, wakiwamo wastaafu walioshika nyadhifa mbalimbali kwenye serikali na vyama vya siasa kukaa nao, tunategemea mchango na maoni yao yatasaidia kuwashawishi viongozi wa vyama vya siasa waangalie upya mifumo ya uteuzi wa wagombea,” alisema.

Alisema lengo la mkutano huo uliokutanisha wadau mbalimbali vikiwamo vyama vya siasa ni kujadili kwa pamoja hatua gani ambazo zinaweza kuchukuliwa ili uteuzi wa wanawake kwenye uongozi na siasa uongezeke.

Naye, mgeni rasmi kwenye mkutano huo, Mbunge wa Vunjo, James Mbatia, alisema yapo Malengo Endelevu ya Dunia 17 yanatakiwa yatekelezwe kwa misingi ya kipaumbele na kuyataja kuwa ni kuondokana na umaskini katika dunia, njaa, afya bora na ustawi wa jamii, elimu bora kwa wote, usawa wa jinsia, majisafi na salama.

“Ili yatekelezwe lazima tuwe na mifumo inayolinda utu wa binadamu, mifumo ya wazi, inayotoa haki, inayohakikisha amani ya dunia inalindwa. Hivyo Tanzania hatuna budi kuhakikisha usawa wa jinsi kama lilivyo lengo la tano, hasa kwa kuwa na utashi wa kisiasa wa kusimamia jambo hilo likaanzia kwenye mazingira ya kielimu,” alisema.