Miche milioni 1.6 ya matunda, mbao kuzalishwa

13Oct 2021
Grace Mwakalinga
Rungwe
Nipashe
Miche milioni 1.6 ya matunda, mbao kuzalishwa

WILAYA ya Rungwe mkoani Mbeya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamepanga kuzalisha zaidi ya miche milioni 1.6 ya mbao, matunda na kivuli ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuhifadhi mazingira wilayani humo.

Akizungumza na Nipashe juzi, Ofisa Maliasili wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Castor Makeula, wakati wa zoezi la uoteshaji wa miche ya kitalu kilichopo Kata ya Bulyaga mjini Tukuyu, alisema miche hiyo itagawiwa bure kwa wananchi kwenye sekta binafsi na umma kwa lengo la kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia biashara ya mbao na matunda.

“Tumeamua kuzalisha miche milioni 1.6 ya aina mbalimbali kama vile matunda, mbao na kivuli ikiwa ni hatua ya kuhifadhi vyanzo vya maji, kilimo na biashara ili kukuza uchumi wa wakazi wa Rungwe sambamba na utunzaji wa mazingira,” alisema Makeula.

Vile vile, alisema kwa sasa wanaendelea kuzalisha miche hiyo na ifikapo Januari 2022 wananchi wataanza kugawiwa kwa kushirikiana na maofisa ugani kutoka kila kata za wilaya hiyo.

Baadhi ya wananchi walisema ni utaratibu mzuri ulioanzishwa na wilaya kuwagawia miche ili kuendeleza jitihada za kuhifadhi mazingira na kwamba wataendelea kuitunza kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

Miongoni mwa wananchi hao, Mary Mwangupili wa Kijiji cha Ilolo alisema ni mara kadhaa amekuwa akipewa miche ya matunda na mbao na viongozi wa wilaya hiyo na ameanza kunufaika kwa kuuza parachichi na kujiingiza kipato.

Aliishukuru serikali na kuishauri kuongeza jitihada kutunza chanzo cha maji cha Mto Kilasi ili kiendelee kutoa maji katika kipindi chote cha mwaka na kupanda miti.

Habari Kubwa