Miezi miwili kiwanda kuzuia vumbi

08Mar 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Miezi miwili kiwanda kuzuia vumbi

KIWANDA cha saruji cha Twiga cha jijini Dar es Salaam kimepewa miezi miwili kuondoa kero ya vumbi inayowasumbua wananchi wanaozunguka eneo hilo, vinginevyo kitafungiwa.

Agizo hilo lililotolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola, lilitokana na ziara ya siku moja kiwandani hapo akiwa ameandamana na maofisa wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira  (NEMC), baada ya kupata taarifa ya uchafuzi wa mazingira kutokana na vumbi zito linalotoka wakati wa uzalishaji saruji.

“Nimesikiliza pande zote na nimejiridhisha kuwa tatizo la vumbi lipo na linaathiri afya za wananchi wanaozunguka kiwanda hiki, hivyo natoa miezia miwili kuanzia leo (juzi) kusiwapo na malalamiko ya vumbi, kinyume cha hapo kiwanda hiki ninakifungia hadi mtakapojirekebisha,” alisema Lugola.

Alisena vilio vya wananchi vinamfikia Rais John Magufuli ambaye alimuamini na kumteua kwa nafasi hiyo, hivyo hawezi kuvumilia kuona wananchi wanapiga kelele ambazo hazipatiwi ufumbuzi wa kudumu.

“Vilevile NEMC nawataka mje kupima vumbi hili mara kwa mara ili mjiridhishe kuwa linakidhi viwango vya kimazingira, lakini pia msisubiri kuletewa majibu ya vipimo kutoka kwa wamiliki wa kiwanda, wao hawawezi kuwaletea majibu mabaya lazima wataegemea upande wao,” alisema Lugola.

 

Kuhusu malalamiko ya wananchi, alimtaka ofisa mazingira wa eneo hilo la Wazo na Ofisa Afya wa Kinondoni watafute eneo la kujenga choo kwa ajili ya wafanuabiashara wa eneo hilo ambao pia walilalamika kiwanda kinamwaga maji katika maeneo yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Twiga Cement, Alfonso Velez, alisema hana namna zaidi ya kupokea maagiza ya Lugola, lakini anaamini kiwanda chake hakuna uchafuzi wa mazingira waliofanya kwa sababu anaamini ndicho kiwanda pekee cha saruji katika ukanda huu kinachotunza mazingira.

Alibainisha wamejitahidi kwa kadiri ya uwezo wao kuwa karibu na wananchi na hata kuwatembelea ambao wanalalamika vumbi linaingia vyumbani mwao kwa lengo la kumaliza tatizo hilo na kwa hakika wamefanikiwa kulipunguza.