Mifugo iliyoshikiliwa Mvomero yalipiwa faini mil. 11/-

15Mar 2016
Idda Mushi
Nipashe
Mifugo iliyoshikiliwa Mvomero yalipiwa faini mil. 11/-

MIFUGO iliyokuwa ikishikiliwa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero baada ya kuingia wilayani humo bila kibali, imelipiwa faini ya Sh. milioni 11.8 na kuachiliwa kuendelea na safari.

Mifugo hiyo iliyokuwa ikishikiliwa kwa takribani siku tano na Uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Mvomero,ililipiwa fidia hiyo kwa mujibu wa sheria,ikiwa ni utekelezaji wa sheria ndogo za halmashauti hiyo baada ya mifugo hiyo kukosa kibali cha kuingia wilayani humo ikitokea Wilaya ya Kilosa, huku ikidaiwa kusafirishwa kwa kuswagwa badala ya kubebwa kwenye magari maalum.

Ofisa Mifugo wa Wilaya ya Mvomero, Daniel Pangani, alisema wamekabidhi mifugo hiyo 366 ikiwa katika hali nzuri kiafya baada ya wamiliki wake kutimiza masharti yote yaliyotajwa kwenye sheria.

Pangani aliahidi kuwa wataendelea kutoa elimu zaidi kwa wafugaji ili kuepusha matatizo na migogoro mbalimbali kujitokeza.

Mmiliki wa mifugo hiyo, Yame Due, pamoja na kukiri kupokea mifugo yake ikiwa katika afya njema, aliiomba serikali kuwaasa wataalam wake kusimamia vyema kazi zao hasa kwa kuhakikisha maofisa mifugo wanayafikia na kuyaelimisha makundi ya jamii ya wafugaji hasa maeneo ya vijijini ikiwamo kuhusiana na sheria za mifugo.

Due alisema bila kufanya hivyo migogoro ya mara kwa mara ya wàfugaji haitakoma.

Wafugaji wengine akiwamo Gabriel Skai na Emmanuel Ami, walisisitiza maofisa hao wa mifugo kuwafikia wàfugaji kwa elimu, huduma na tiba wakati wote badala ya kusubiri wanapopata matatizo ndipo wanaposogea jirani nao.

Habari Kubwa