Mikoa 2 yabeba jukumu mafuta

14Jun 2018
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Mikoa 2 yabeba jukumu mafuta

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo, amesema mikoa ya Dodoma na Kigoma ina wajibu wa kuisaidia nchi kuondokana na tatizo la upungufu wa mafuta ya kupikia kwa kuwa ni maarufu kwa uzalishaji wa mazao ya alizeti, karanga na michikichi.

Jafo alitoa kauli hiyo  alipokuwa akifungua mkutano wa kuboresha mazingira ya biashara kwa uwekezaji endelevu na kukuza biashara kwa mikoa hiyo.

 

Alisema ni vyema yakatumika mabaraza ya biashara ya mikoa hiyo kuisaidia nchi kuondokana na matumizi ya fedha nyingi kwenye uangizaji wa mafuta.

 

“Hivi karibuni kulikuwa na upungufu wa mafuta, hivi hamuoni kuwa haya mabaraza yana umuhimu wake kwa kuwa hii mikoa mnaweza kupanga mikakati ya kuzalisha mafuta na kuacha kuagiza nje ya nchi, Dodoma na Kigoma mnaweza kutusaidia kwenye hili,” alisema juzi.

 

Aidha alisema kumekuwapo kutowajibika ipasavyo kwa viongozi wa mabaraza ya biashara hali inayosababisha wafanyabiashara kufikisha malalamiko yao ngazi ya juu.

 

“Hoja nyingi zilinazojadiliwa katika vikao vya juu zilipaswa ziishie ngazi ya mamlaka ya serikali za mitaa, lakini inaoenekana huko hayakufanyiwa kazi na inadhihirisha kwamba mabaraza hayatekelezi wajibu wao ipasavyo,” alisema.

 

Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, alisema mkoa huo una fursa kubwa ya kilimo cha alizeti kustawi na kwamba wataendelea kuhamasisha wakulima kujikita kwenye kilimo hicho.

Alisema mafuta ya alizeti kwa sasa yamepanda bei kutokana na kuwapo na uzalishaji mdogo kwa kuwa watu badala ya kujikita kwenye kilimo ili kuwa na malighafi ya kutosha wamekimbilia kuwekeza kwenye viwanda.

Dk. Mahenge aliwataka wakulima kulima zaidi kwa kuwa soko la zao hilo lipo.

 

Habari Kubwa