Mil. 108/- zachangwa kujenga hospitali Kigoma

07Feb 2016
Emmanuel Matinde
Nipashe Jumapili
Mil. 108/- zachangwa kujenga hospitali Kigoma

ZAIDI ya Sh. Milioni 38 zikiwamo fedha taslimu, ahadi, hundi pamoja na mifuko ya saruji tani moja, vimechangwa katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Hospitali ya Rufaa inayotarajiwa kujengwa mkoani Kigoma.

Kiasi hicho kimefikisha Sh. Milioni 108, ambazo zimechangwa kupitia harambee mbalimbali inayosimamiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali (mstaafu), Issa Machibya, viongozi wa halmashauri zote za mkoa huo, wakuu wa wilaya, viongozi wa dini, siasa na watumishi wa umma.

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa harambee hiyo, Mganga Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Dk. Leonard Subi, alisema hospitali inayotarajiwa kujengwa itakuwa kubwa ya kisasa, itakayowaondolea shida wananchi wanaotumia gharama kubwa kusafiri nje ya mkoa huo kupata huduma.

Dk. Subi alisema mwaka 2015, wananchi 1,600 walipatiwa rufaa kwenda hospitali ya Taifa Muhimbili, hospitali ya rufaa Bugando na KCMC kwa gharama ya jumla ya Sh. Bilioni 5.2.

Aidha, Dk. Subi alisema Sh. Trillioni 4 zinahitajika ili kukamilika kwa ujenzi wa hospitali hiyo, na iwapo kila mwananchi wa mkoa wa Kigoma atachangia Sh. 100 kila wiki, katika kipindi cha mwaka mzima zitapatikana Bilioni 11.9.

Katika harambee hiyo, mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kakonko, Jaina Saidi, mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kibondo, Saimon Kanguye na mdau wa huduma za afya, Salvatory Chobaliko, walikuwa miongoni mwa waliochangia ujenzi wa hospitali hiyo.

Awali katika hotuba yake ya kuwakaribisha wadau kwenye harambee hiyo, Machibya alisema ujenzi wa hospitali hiyo utaendeleza mkoa kiuchumi na kwamba nchi jirani zitapata huduma za matibabu.

Habari Kubwa