Mkaa fursa kwa pato la Taifa

06Dec 2017
Christina Haule
Nipashe
Mkaa fursa kwa pato la Taifa

SERIKALI itanufaika na pato la Dola za Marekani bilioni moja kila mwaka sawa na Shilingi trilion 2.2, iwapo itazingatia uzalishaji endelevu wa mkaa na kuuwekea mfumo rasmi, wadau wa sekta ya misitu wameeleza.

Ofisa Mradi katika Mtandao wa Jamii ya Usimamizi wa Misitu Tanzania (Mjumita) maarufu kama ‘mkaa endelevu,’ Charles Leonard, alitoa ufafanuzi huo mwishoni mwa wiki alipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa kuelezea umuhimu wa sekta hiyo.

Mjumita, ni kati ya asasi nne zinazoshirikiana na ubalozi wa Uswisi, inayowakilishwa na Shirika la Ushirikiano na Maendeleo la Uswisi (SDC), katika kuendesha miradi ya mkaa endelevu wako katika wilaya za Kilosa na Morogoro Vijijini.

Asasi zingine zilizoko katika harakati zinazoendesha mradi huo ni Shirika la Kuhifadhi Misitu Asilia Tanzania (TCFG), Shirika la Kuendeleza Nishati Asilia na Maendeleo (TaTEDO).

Alisema, kasoro iliyopo ni kwamba Sera ya Nishati kitaifa haiipi nafasi mkaa na inazingatia zaidi mbadala wa gesi na umeme, huku kukikosekana mfumo rasmi na endelevu wa kuhudumia nishati hiyo kongwe.

Leonard alisema nishati ya mkaa inaonekana inaharibu mazingira sambamba na kuteketeza maliasili ya misitu kwa takribani hekta 500,000 kila mwaka, lakini ikitumika vizuri vyema na mapato yake kuingizwa katika mifumo sahihi, italiingizia Taifa pato hilo rasmi .

Alisema huo umesababishwa kutokuwapo kwa sera madhubuti ya kusimamia nishati ya mkaa  na kwamba nishati hiyo, huku nishati hiyo ikiendelea kutumiwa na wananchi wengi nchini hususan wa kipato cha chini. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Mjumita, Rehema Njaidi, alisema licha ya kuwa na sera isiyo madhubuti ya kusimamia misitu nchini, lakini ipo njia sahihi ya mkaa endelevu ambayo ikiwafikia wananchi kusaidia utunzaji misitu, sambamba na kuinua uchumi wa wananchi wanaojihusisha na shughuli ya uvunaji wa misitu.

Kwa mujibu wa pendekezo la andiko la Sera ya Misitu kutoka kwa wadau hao, inayofanyiwa kazi ya marekebisho na serikali, ikiwa katika hatua ya kupokea maoni.

Leonard alisema hadi sasa hakuna matarajio Watanzania kuhamia katika nishati mbadala ya gesi na umeme inayopendekezwa katika kipindi cha wastani wa miaka 20 ijayo, kutokana na uhalisia wa umasikini wao, huku watumiaji wakiwa kundi kubwa la wananchi.