Mkaa sasa basi Dar

30Aug 2016
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Mkaa sasa basi Dar

SERIKALI inakusudia kusambaza gesi katika Jiji la Dar es Salaam ili kupunguza matumizi makubwa ya mkaa yanayoongoza kitaifa.

Hayo yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Richard Muyungi wakati wa kikao cha Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira.

Kamati hiyo ilikuwa ikipokea na kujadili taarifa ya mikakati ya utekelezaji wa mipango endelevu ya ofisi hiyo.

Alisema Jiji la Dar es Salaam hutumia wastani wa magunia 500,000 ya mkaa kwa mwezi, hivyo kuwa kinara kwa matumizi ya nishati hiyo kitaifa.

Kwa msingi huo, Muyungi alisema ofisi hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), ina mpango wa kuanzisha mradi wa kusambaza gesi Dar es Salaam.

Alisema mradi huo utagharimu dola milioni 117 za Marekani (sawa na Sh. bilioni 140).

“Tunataka kupunguza matumizi ya mkaa, tunataka tufanye kama TPDC walivyofanya kwenye kila nyumba ya mfanyakazi inatumia gesi asilia, tunataka tuchague maeneo ya mfano kufanya hivyo, tumefanya utafiti ili kufanikisha inahitajika fedha hizo,” alisema Muyungi.

Aidha, alisema matumizi ya fedha hizo ni pamoja na kujenga miundombinu ya mabomba kwenye nyumba ili kupitisha gesi hiyo kama ilivyo mabomba ya maji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Dalaly Kafumu, ambaye pia ni Mbunge wa Igunga, alisema kuna umuhimu wa kuifanyia marekebisho Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Dk. Kafumu aliitaka wizara hiyo kutengeneza mradi wa kuhakikisha gesi asilia inatumika nchini ili kuondokana na matumizi ya mkaa.

Habari Kubwa