Mkaa waiingizia Kilosa ushuru wa mil. 290/-

08Sep 2016
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Mkaa waiingizia Kilosa ushuru wa mil. 290/-

UTEKELEZAJI wa mradi wa kuleta mageuzi katika sekta ya maliasili umesaidia kuongeza mapato katika Wilaya ya Kilosa, mkoani hapa,baada ya kukusanya ushuru wa Sh. milioni 290, uliotokana na mkaa.

Fedha hizo zilizokusanywa kutokana na ushuru wa mkaa zimesaidia kupunguza changamoto mbalimbali za miundombinu iliyokuwa ikiwakabili.

Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Hassan Kambega,alisema hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa awamu ya pili katika Wilaya ya Mvomero na Morogoro.

Mradi unatekelezwa na Shirika la kuhifadhi misitu asili Tanzania (TFCG), kwa kushirikina na Shirika la kuendeleza nishati asilia Tanzania (TaTEDO), kwa ufadhili wa Shirika la maendeleo na ushirikiano la Uswis (SDC).

Alisema,fedha hizo zimeweza kujenga barabara, nyumba ya mwalimu, mganga, ofisi za vijiji na kuwalipia bima ya afya ya jamii wananchi wa vijiji 10 vilivyoingizwa katika mradi huo.

Alisema pamoja na hayo mradi huo umeweza kuokoa hekta 16 ya misitu iliyokuwa ikikatwa kila mwaka kwa ajili ya kuchomwa mkaa.

Aliitaja miti iliyokuwa ikikatwa kiholela na usiokuwa endelevu ni pamoja na miyombo inayotumika kuchomwa mkaa.

Alisema nishati ya mkaa imekuwa ikitumiwa kwa kiasi kikubwa kwenye matumizi ya kupikia kuliko nishati nyingine na kuwataka wananchi wakiwamo wachoma mkaa wapewe elimu.

Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la kuhifadhi misitu asili Tanzania (TFCG), Charles Meshack, alisema zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania, hususani wanaoishi mijini, wanatumia nishati ya mkaa kwa matumizi ya jikoni.

Hata hivyo, alisema licha ya kugunduliwa kwa gesi, baadhi ya wananchi wanashindwa kumudu gharama za kununua gesi hiyo na kulazimika kununua mkaa.

Meshack, alisema pamoja na kuwapo kwa matumizi makubwa ya mkaa, bado hakuna sera inayosimamia nishati hiyo hali inayosababisha halmashauri nyingi kupoteza mapato yanayotokana na mkaa.

Meneja mradi wa TFCG, Charles Leonard, alisema mradi huo, utakuwa wa miaka minne na ulianza Desemba 2015 hadi Novemba 2019.

Alisema mradi huo unalenga kuanzisha mfumo wa usimamizi endelevu wa mnyororo wa thamani wa mkaa na mazao mengine ya misitu katika vijiji 30 wilayani Kilosa, Mvomero na Morogoro.

Awali akizindua mradi huo,Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo, alisema kama hakutafanyika mabadiliko katika sekta ya mkaa, misitu ya asili itapotea na hali ya mazingira itaharibika.