Mkakati kukabili 'mawimbi' angani

15Mar 2017
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mkakati kukabili 'mawimbi' angani

KAMPUNI ya usafiri wa ndege ya Fastjet, imesema iko mstari wa mbele kupambana na changamoto zinazoizunguka sekta ya usafiri wa anga ili kuhakikisha inawapatia huduma bora wateja wake.

Mkuu wa Masoko na Mahusiano wa kampuni hiyo, Lucy Mbogoro.

Mkuu wa Masoko na Mahusiano wa kampuni hiyo, Lucy Mbogoro, aliyasema hayo alipokuwa akitangaza mafanikio ya kampuni hiyo tangu ilipoanza kufanya safari zake nchini, ambapo "imekwishasafirisha wateja milioni 2.4".

“Katika sekta ya anga, kuna changamoto nyingi na sisi kama kampuni ya ndege ya bei nafuu tumesimama imara kupambana nazo tangu tulipoanza kutoa huduma nchini, hiyo ikiwa ni Novemba 2012,” alisema Mbogoro.

Aliongeza kwamba tangu wakati huo, Fastejet imeweza kusafirisha wasafiri 2.4 milioni kupitia safari 26,629 ambazo ndege zake zimefanya.

“Kwa sasa Fastjet imeajiri Watanzania zaidi ya 150, ambao wanafanya kazi moja kwa moja na kampuni yetu, lakini nje ya hapo kuna watu wengi zaidi ambao wanafaidika na Fastjet,” alisema Mbogoro.

“Kwa sasa tunafanya safari 117 kwa wiki, tukisaidia kujenga uchumi wa nchi yetu kwa kusafirisha bidhaa na malighafi mbalimbali, lakini pia tukiunganisha ndugu, jamaa na marafiki na pia watalii kwa kuwapatia usafiri wenye hadhi ya juu kwa bei nafuu ambayo kila Mtanzania anaimudu."

Kwa sasa Fastjet inaruka kutokea Dar es Salaam kuelekea mikoa ya Kilimanjaro, Mbeya na Mwanza, na kwa upande wa safari za kimataifa Fastjet inaruka kuelekea miji ya Lusaka, Zambia na Harare nchini Zimbabwe.

Mbogoro alisisitiza kuwa, Fastjet itaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na serikali katika kuhakikisha mipango yote ya uwekezaji inaenda sawa, huku ikishirikiana na watendaji wote wanaohusika katika kuongeza nafasi za ajira kwa Watanzania.

Habari Kubwa