Mkakati kuongeza uzalishaji chai waja

22Feb 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Mkakati kuongeza uzalishaji chai waja

SERIKALI imekuja na mikakati ya kuongeza uzalishaji wa zao la chai na kudhibiti upotevu wake kwa kuanzisha mnada na ujenzi wa viwanda vya kusindika jirani na mashamba ya wakulima.

Mnada huo unatarajiwa kuanzishwa nchini mwaka huu mijini Dar es Salaam ili wakulima waondokane na adha wanayoipata ya kusafirisha chai kwa gharama ya zaidi ya Sh.Milioni sita kwenda Mombasa nchini Kenya kwenye soko la zao hilo.

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki Jijini hapa katika kikao chake na viongozi wa vyama vya msingi 41 vya sekta hiyo ya chai.

Alisema kikao hicho kinatokana na sekta ya kilimo kupata ufadhili kutoka Umoja wa Ulaya(EU) wa EURO milioni 100 ambazo kwa asilimia kubwa zinalenga kupaisha uzalishaji wa zao hilo na kuwa na tija kwa wakulima.

Alibainisha kuwa serikali imeweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo kutoa tani 25,000 hadi kufikia tani 60,000 ifikapo mwaka 2024 kwa kuhakikisha wakulima wanapatiwa pembejeo na uhakika wa masoko kwa njia ya mnada.

“Kati ya fedha hizo tulizopata ufadhili, EURO milioni 48 zitajenga miundombinu ya barabara za mashambani ili kuondoa tatizo la kushindwa kufikisha chai sokoni,”alisema.

Bashe alisema uzalishaji wa chai ni mkubwa kuliko uwezo wa viwanda vya Tanzania kuchakata chai.

“Tayari kuna mazungumzo yanafanyika na kampuni kubwa mbili za duniani ambazo zinanunua chai Mombasa nchini Kenya zimekubali kufungua matawi yake ili kushiriki kwenye mnada wa chai ambao unatarajiwa kabla ya mwisho wa mwaka huu uwe umeanza.” alisema.

Pia alisema ili kuondokana na tatizo la upotevu wa chai mradi huo utasaidia kujengwa kwa viwanda vidogo vya kuchakata chai karibu na mashamba ya chai.

Naibu Waziri huyo, alisema kwenye kikao hicho wamejadiliana mfumo wanaotumia wakulima kupata Pembejeo na kuwataka wakulima wote nchini kuagiza mbolea kupitia vyama vyao vya ushirika ili kupata kwa bei nafuu na kwa mkopo.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania, Nicholaus Mauya, alisema kumekuwapo na upotevu wa chai unaotokana na kuharibika wakati wa usafirishaji na kutovunwa kutokana na kukosa viwanda vya kununua.

Alisema mkakati wa kujenga viwanda jirani na wakulima ni utaratibu unaotumika nchini India na umefanikiwa kuwa na tija.

“Uzalishaji wa chai hutegemea hali ya hewa na kuna misimu miwili ambapo uzalishaji mkubwa huwa msimu wa mvua na kusababisha chai nyingi kuharibika, kwa mfano kwa mwaka 2019/20 upotevu wa chai ulikuwa tani 2000,” alisema.

Habari Kubwa