Mkakati kupunguza uagizaji wa mafuta ya kula waibuliwa

25Jun 2019
Ashton Balaigwa
MOROGORO
Nipashe
Mkakati kupunguza uagizaji wa mafuta ya kula waibuliwa

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) imeanza mkakati wa kupunguza  uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi  baada ya kuanza kuzalisha  mbegu za alizeti zilizothibitishwa ubora kwa ajili ya kutumiwa na wakulima na hatimaye kuzalishwa kwa wingi.

Kupitia mkakati huo tayari Kituo cha Utafiti wa Kilimio Ilonga, Kilosa mkoani Morogoro, kimepewa jukumu la kuzalisha mbegu hizo za alizeti ikiwamo ya rekodi ambayo imeanza kutumika kwa wakulima.

Akizungumza katika Siku ya Maonyesho ya Kilimo Biashara yaliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Tari na Baraza la Nafaka la Ukanda wa Afrika Mashariki, Mtafiti wa Alizeti nchini, Frank Reuben, alisema kwa mwaka huu wameshazalisha mbegu ya alizeti aina ya Rekodi tani 37.8 ambazo zimeshasambazwa kwa wakulima.

Alisema kupitia uzalishaji mbegu hizo, ekari 18,500 zitapandwa na wakulima katika mikoa mbalimbali ya uzalishaji wa alizeti ikiwamo Singida, Dodoma na Morogoro ambayo imewekewa mkakati wa kulima zao hilo.

Mtafiti huyo alisema kupitia mkakati huo, Tari imepanga kutoa utafiti mwingine wa mbegu ya alizeti itakayokuwa na ubora kuliko mbegu yoyote iliyoko sokoni kwa sasa ili kuongeza uzalishaji wa mafuta maradufu.

"Tari inaendelea na utafiti wa mbegu zingine nne za alizeti kwa ajili ya kuhakikisha uzalishaji wa mafuta unaongezeka hapa nchini," alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tari, Dk. Geofrey Makamilo, alisema kabla ya kuanzishwa kwa Tari, Kituo cha Utafiti cha Ilonga kilikuwa kinazalisha wastani wa tani 2.3 za mbegu za alizeti lakini kwa mwaka wa kwanza baada ya kuundwa kwa taasisi hiyo, uzalishaji wa mbegu umeongezeka na kufikia tani 7.5.

Dk. Mkamilo alisema mkakati wa Tari ifikapo mwaka 2020- 2022 ni kufikisha tani milioni 1.5 za alizeti ambazo zitakuwa na uwezo wa kutoa mafuta ujazo wa tani 600,000 hivyo kupunguza kwa kiwango kikubwa cha uagizaji wa mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.

Mmoja wa wakulima wa alizeti na mzalishaji wa mafuta, Khalifan Hamad, kutoka kata ya Magomeni wilayani Kilosa, alisema mbegu ya ‘Rekodi’ iliyofanyiwa utafiti na Tari Ilonga imeonyesha kuzaa vizuri na ubora mkubwa utakaosaidia kuongeza uzalishaji wa mafuta nchini.

Alisema kuwapo kwa kituo cha utafiti pia kumewasaidia kupata ushauri na utaalamu wa kilimo bora cha alizeti tofauti na awali walikuwa wakipanda holela na kukosa mavuno ya kutosha.

Akifungua maonyesho hayo, Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, alisema Tari Ilonga ina wajibu wa kuendeleza utafiti katika mazao mengine ya jamii ya nafaka yakiwamo mtama, uwele, ulezi, mbaazi, kunde, choroko, soya, dengu na njugu mawe.

Habari Kubwa